Makonda aanza ziara FC Barcelona

BARLEONA: WAZIRI Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameanza ziara maalum ya siku nne katika Klabu ya FC Barcelona nchini Hispania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutafuta fursa za ushirikiano zitakazochangia maendeleo ya soka nchini Tanzania.
Ziara hiyo, iliyoanza Septemba 14, 2026, imefanyika kwa mwaliko wa Rais wa FC Barcelona, Joan Laporta, ambapo Waziri Makonda amefanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo kuhusu maeneo mbalimbali yenye fursa ya ushirikiano kati ya Barcelona na Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zimeangazia namna ya kuimarisha maendeleo ya soka kupitia ukuaji na uendelezaji wa vipaji, mafunzo na maendeleo ya kiufundi, pamoja na uzoefu katika uendeshaji na uendelezaji wa timu za taifa.
Aidha, ziara hiyo imelenga pia kubaini namna uzoefu na utaalamu wa FC Barcelona unavyoweza kutumika katika kuunga mkono maandalizi ya Tanzania kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambalo Tanzania ni miongoni mwa wenyeji.
Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua milango ya fursa zaidi kwa vijana wenye vipaji vya soka nchini, pamoja na kuimarisha maarifa na mifumo ya maendeleo ya soka kwa kuangalia uzoefu wa moja ya klabu kubwa na zenye historia katika maendeleo ya mchezo huo duniani.
Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Rais wa FC Barcelona, Joan Laporta, ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia msiba wa Mume wake, Mzee Hafidh Ameir Hassan, aliyefariki dunia Septemba 7, 2026.
Ziara hiyo ya siku nne inaendelea nchini Hispania, huku ikilenga kuimarisha mahusiano na kutengeneza fursa mpya za kimkakati katika sekta ya michezo, hususan maendeleo ya soka nchini Tanzania.




