Clara: Nina mtihani mkubwa mbele yangu

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI mpya wa Washington Spirit ya Marekani, Clara Luvanga ameeleza kuwa mchezaji ghali duniani ni faraja lakini pia ni mtihani mkubwa kwake kuelekea msimu mpya.
Clara amezungumza hayo baada ya kuvunja rekodi ya usajili kwa wachezaji wanawake akisajiliwa kwa kitita cha Dola milioni 2.3 kutoka Al Nassr ya Saudia kuelekea Washington.
Mshambuliaji huyo alisema wadhifa huo pia una changamoto zake kwani sasa atalazimika kuonesha ubora wa thamani hiyo na huo ndio mtihani mzito anaopaswa kupambana nao kwa sasa.
“Najisikia furaha kuwa mchezaji wa thamani zaidi lakini kuna ugumu ambao unakuja, utafurahia kwa sababu zimewekwa namba za hela lakini kuna wachezaji ambao wapo Chelsea, Bayern (Munich), Real Madrid, Barcelona na kwingine.
“Sasa hizo namba zilikuja kwa kile ulichokionesha na sasa inapaswa kuonesha zaidi ya hao wengine, uwe na ubora wa kuendana na hizo namba na kuendelea kuwazidi wengine kama hao ambao wapo timu kubwa na maarufu zaidi.
“Kwa hiyo kwangu huo ni mtihani, na lazima nifanye vizuri ili niendane na thamani niliyopewa. Kwa hiyo ni kupambania kuendelea kuonesha thamani zaidi ya wengine ambao wapo klabu kubwa lakini hawajafika hapo,” alisema Clara.
Aidha, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga Princess ya Dar es Salaam amesema akili yake ameielekeza kwenye kituo chake kipya cha kazi kujua timu inataka nini na yeye aweke vipi malengo yake binafsi.
“Kwa sasa napaswa kufahamu kwenye kituo changu kipya kocha anahitaji nini kwangu, halafu kuhakikisha nasaidia malengo ya timu na mwisho kupambana kutafuta namba ninazozihitaji mimi binafsi, ” alisema Clara.
Aidha, Clara, 21 amewatia moyo wachezaji wanaopambana nje ya nchi kuendelea kupigania ndoto zao licha ya kupitia changamoto nyingi za upweke wa lugha, kukaa mbali na familia kwa muda mrefu na mengineyo.
Amesisitiza haipaswi kushindwa kirahisi kupambana nje ya nchi kwani unaporejea nyumbani ni wazi umekubali kurudi hatua nyingi nyuma na kuyapa mgongo mafanikio ya kimataifa.




