Taifa Queens nendeni mkaipambanie bendera ya taifa

DAR ES SALAAM: OFISA Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, ameitaka Timu ya Taifa ya Netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, kwenda nchini Kenya ikiwa na dhamira ya kupambana na kutafuta nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia la Netiboli litakalofanyika mwakani nchini Australia.
Maguzu ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuikabidhi Taifa Queens bendera ya Taifa, kabla ya timu hiyo kuondoka leo kuelekea Kenya kushiriki Mashindano ya Afrika ya Kufuzu Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 19 hadi 26, 2026.
Amesema ushiriki wa mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia ni jambo kubwa kwa Tanzania, hivyo amewataka wachezaji kutumia fursa hiyo kupambana kwa nguvu zote na kuiwakilisha nchi kwa heshima.
“Nendeni mkapambane, ushiriki wa mashindano ya Dunia si kazi ndogo, ni shughuli kubwa,” amesema Maguzu.
Maguzu amewataka Watanzania na wadau wa michezo kuendelea kuwaunga mkono wanamichezo wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kuweka mbele maslahi ya Taifa wanapokuwa nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania, Rahma Kilimba, amesema kikosi cha Taifa Queens kinaundwa na wachezaji 14 ambao wataiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.
Rahma amesema maandalizi ya timu yamekwenda vizuri, ambapo kikosi hicho kiliingia kambini Septemba 2 na kuendelea na mazoezi hadi Septemba 17, 2026, kabla ya kuvunja kambi jana.
Naye Nahodha wa Taifa Queens, Jesca Julius, amesema wachezaji wako tayari kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha Tanzania inapata matokeo mazuri na kufungua njia ya kushiriki Kombe la Dunia la Netiboli mwakani nchini Australia.




