Ngorongoro Heroes kuchuana na Ethiopia

DAR ES SALAAM: TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Ngorongoro Heroes inatarajia kuendelea na kampeni ya kufuzu AFCON dhidi ya Ethiopia kesho katika mchezo wa Kanda ya Cecafa utakaochezwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam
Ngorongoro Heroes, tayari imeanza kwa ushindi baada ya kuifunga Rwanda katika mchezo wake wa kwanza mabao 3-0 na sasa itakutana na Ethiopia kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF Clifford Ndimbo: “TFF imewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo, ambayo inapigania tiketi ya kushiriki fainali za AFCON kwa vijana chini ya miaka 20,”
Wakati huo huo, timu ya taifa ya futsal ipo kambini ikiendelea na maandalizi ya AFCON 2026 itakayofanyika Morocco. Kikosi hicho kinatarajiwa kuelekea nchini humo Oktoba Mosi, ambako kitapata nafasi ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kuanza kwa mashindano.
Kwa upande wa soka la ufukweni, Tanzania inajiandaa kukutana na Msumbiji katika mechi za kufuzu AFCON. Mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa Dar es Salaam Oktoba 11, huku marudiano yakipangwa kufanyika Maputo kati ya Oktoba 16 na 18.
Tanzania inalenga kupata nafasi ya kushiriki tena fainali hizo, baada ya kushiriki mashindano ya AFCON ya soka la ufukweni mara kadhaa.
Katika maandalizi ya Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 litakaloanza Novemba 19 nchini Qatar, Serengeti Boys inaendelea na kambi Dar es Salaam.
TFF pia inaendelea na mipango ya kuipeleka timu hiyo England kwa kambi ya nje, ambako inatarajiwa kucheza mechi nne za kirafiki kuanzia Septemba 28. Tarehe ya safari itatangazwa baada ya taratibu za maandalizi kukamilika.
Kwa upande wa timu ya taifa ya wanawake, Tanzania inajiandaa na michezo ya kufuzu Olimpiki dhidi ya Botswana. Mchezo wa kwanza utachezwa ugenini Oktoba 9, kabla ya marudiano kufanyika Oktoba 13.
Nayo timu ya taifa ya wanaume chini ya miaka 23 inatarajiwa kuingia kambini leo kwa ajili ya maandalizi ya mechi mbili za kufuzu AFCON U23 dhidi ya Kenya.
Mchezo wa kwanza utachezwa Septemba 28 kwenye Uwanja wa Nyayo, Kenya, saa tisa alasiri, huku mchezo wa marudiano ukipangwa Oktoba 10 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, saa 10 jioni.
Baada ya kuingia kambini, wachezaji wanatarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.




