Bundesliga

Kideo’ champonza kiungo Bundesliga

MOENCHENGLADBACH: Kiungo wa Borussia Moenchengladbach Florian Neuhaus amepigwa faini na kufukuzwa kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo baada ya kuvuja video akionekana kumkejeli mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Bundesliga.

Katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, Neuhaus alionekana akizungumza na watu kadhaa waliovalia vifaa vya Gladbach kuhusu mkurugenzi wao wa michezo Roland Virkus.

Mchezaji huyo mwenye miaka 28 alionekana kumwita Virkus “meneja mbaya zaidi duniani” na akarejelea ushawishi wa mkurugenzi huyo wa michezo katika kuamua mshahara wake wa euro milioni nne kwa mwaka.

Klabu imesema imemtoza faini “nzito” Neuhaus na kumsimamisha kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza kwa wiki nne, huku gazeti la kila siku la Ujerumani la Bild likiripoti kuwa faini hiyo inafikia takriban euro laki moja.

“Tabia na kauli za Florian Neuhaus zinaharibu taswira ya klabu na hazikubaliki, Ameiharibu klabu kwa maneno yake na kuwakatisha tamaa sana watu wanaohusika, jambo ambalo haliendani na maadili ya klabu ” Mkurugenzi Mtendaji wa Gladbach Stefan Stegemann amesema katika taarifa ya klabu hiyo.

Neuhaus alijiunga na Gladbach mwaka 2017 na amecheza zaidi ya mechi 200 katika mashindano yote kwa klabu hiyo, lakini alionekana kama mchezaji wa akiba msimu uliopita na alicheza mechi 17 pekee kwenye ligi huku wakimaliza nafasi ya 10.

Related Articles

Back to top button