Kasiga ahimiza nidhamu kwa wasanii wa filamu

DAR ES SALAAM: KATIBU Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga, amesema tofauti kubwa kati ya kizazi cha sasa cha waigizaji na vizazi viwili vilivyotangulia ni kiwango cha nidhamu kilichojengwa kupitia vikundi mbalimbali vya sanaa hapo awali.
Dk Kasiga ameeleza kuwa zamani wasanii walipitia mafunzo na makuzi ya sanaa ndani ya vikundi maalum, hali iliyowajengea nidhamu, uwajibikaji na uelewa mpana wa tasnia hiyo.
Amefafanua kuwa kwa sasa, kutokana na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na kuongezeka kwa ushawishi wa utandawazi, mtu yeyote anaweza kujitambulisha na kufanya kazi kama muigizaji bila kupitia mafunzo rasmi kama ilivyokuwa zamani.
Kwa mujibu wake, hali hiyo imeifanya Bodi ya Filamu Tanzania kuwa na jukumu kubwa zaidi la kuhakikisha wanatasnia wanazingatia maadili, mila na utamaduni wa Mtanzania katika kazi zao.
“Ni muhimu kwa wasanii kufuata maadili ya kazi yao ili kujenga taswira chanya mbele ya jamii,” amesema Dk Kasiga.
Ameongeza kuwa uzingatiaji wa maadili utawasaidia waigizaji kujijengea heshima, kuaminika katika jamii, pamoja na kupata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa mabalozi wa chapa za kibiashara na kushiriki katika kampeni za kuelimisha umma.
Aidha, amewataka wanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza kutumia ipasavyo mazingira mazuri yaliyopo nchini kwa kufanya kazi zao kwa weledi na staha.
Amesema kufanya hivyo kutaiwezesha serikali, kupitia Bodi ya Filamu Tanzania, kuelekeza nguvu zaidi katika kuboresha miundombinu ya tasnia hiyo na kuongeza ubora pamoja na tija ya kazi za sanaa nchini.




