EPL

Kamari yamponza Paqueta na familia yake

BRAZIL: Ndugu wa kiungo zamani wa WestHam Lucas Paqueta wanaripotiwa kuwa katika uchunguzi wa mamlaka nchini Brazil kuhusu malipo ya benki yaliyotolewa kwa mchezaji mwingine wa Brazil, huku ndugu yao akiwa bado anakabiliwa na mashtaka ya kupanga matokeo.

Tovuti ya habari ya nchini Brazil UOL imeripoti kuwa mjomba wa Paqueta aitwaye Bruno Tolentino na mwanaye Yan Tolentino walikiri kufanya malipo mawili kwa mchezaji wa zamani wa Real Betis, Luiz Henrique, mapema mwaka 2023 akisema kuwa yalikuwa mkopo na hayahusiani na biashara yeyote haramu.

“Nawezaje kusema? Ni pesa alizonidai, alikuwa amenikopesha. Tulikubaliana kuilipa na tukafanya hivyo na nilipokuwa na pesa za kurudisha, nililipa” amesema Bruno

Malipo hayo, ambayo ni zaidi ya pauni 5,000, yalifanywa muda mfupi baada ya fowadi huyo wa Brazil kupewa kadi mbili za njano zenye utata na kufungiwa katika mechi mbili akiwa na Real Betis ya Spain jambo ambalo lilipelekea FA ya Spain kuanzisha uchunguzi wa uwezekano wa upangaji matokeo ikimhusisha mchezaji huyo.

Kwa mujibu wa UOL Tolentino alikiri kwamba ameshinda pesa nyingi kwenye dau alizoweka kwenye mechi zinazomhusisha Henrique, lakini akakana ‘kutonywa’ kabla.

Utata unaozunguka kadi za njano za Henrique umehusishwa kwa karibu na uchunguzi wa FA ya England kuhusu kuhusika kwa Paqueta katika shughuli kama hizo za upangaji matokeo.

Mashtaka dhidi ya Paqueta yanaripotiwa kuwa yanajumuisha makosa manne ya upangaji matokeo, makosa ambayo yanaweza kusababisha mazito kwa kiungo huyo raia wa Brazil.

FA wanadai kuwa Paqueta ‘alibet’ katika mechi za ligi kuu ya England dhidi ya Leicester, Aston Villa, Leeds na Bournemouth ili yeye au marafiki zake wanufaike na dau alizowekewa akipewa kadi.

Mtandao wa Daily mail wa England unadai kuwa mienendo ya kikamari inayotiliwa shaka inayowahusisha Paqueta na Henrique iliripotiwa kuibuliwa na Betway, kampuni ya betting inayodhamini West Ham.

Inaaminika kuwa dau nyingi zenye kutiliwa mashaka zinazomhusisha Paqueta ziliwekwa na watu wa familia yake, jambo lililofanya uchunguzi kuwa mgumu zaidi. Tayari Paqueta na Henrique kupitia mawakala wao wamekanusha shutuma hizo.

 

Related Articles

Back to top button