Burudani

Hollywood kwa moto haswa!

Keanu Reeves aingia kwenye mbio za magari

MWIGIZAJI mashuhuri wa filamu, Keanu Reeves amehamia kwenye mbio za magari kuonesha ujuzi wake mwingine.

Keanu anayefahamika kwa mapigano ya kung-fu kupitia filamu za John Wick, ameonekana wikiendi iliyopita akifanya mazoezi ya mashindano hayo.

Imeelezwa Reeves anajiweka sawa kwa ajili ya michuano ya kila wikiendi ya Kombe la GR.

Keanu alionekana akijifua na gari namba 92, Eagles Canyon Racing Toyota GR 86 akionesha umakini wa hali ya juu katika mafunzo hayo.

Ingawa hii ni mara ya kwanza kwa Keanu katika mashindano hayo lakini ameonesha ufundi mkubwa wa kuendesha gari kwa kasi kwenye John Wick 4 na hata alipoendesha Toyota Grand Prix hivi karibuni huko Long Beach katika mashindano ya mastaa mbalimbali.

Lil Durk atabiriwa mazuri

BAADA ya rapa Lil Durk kujitosa kwenye uigizaji ametabiriwa kuwa anaweza kufanya makubwa siku za usoni kutokana na uwezo alioonesha.

Hivi karibuni, Durk ameonekana kwenye sehemu ya mwisho ya tamthilia maarufu ya Power Book II: Ghost iliyo chini ya rapa 50 Cent.

Mwigizaji muhimu kwenye tamthilia hiyo, LaToya Tonodeo aliyevaa uhusika wa Diana Tehada amesema kwa kipaji alichoonesha msanii huyo ni kama milango imefunguka kwake katika tasnia hiyo.

Naye, Durk anayeendelea kufanya vizuri na wimbo wa All My Life aliomshirikisha J.Cole, ameonesha kufurahishwa na uigizaji huo kwa kuweka mtandaoni picha mbalimbali akiwa na mastaa wa tamthilia hiyo.

Aidha, Power Book II: Ghost imefikia mwisho lakini fununu zinaeleza inaweza kuendelea kwa upande wa maisha mengine, hivyo Durk pia anaweza kuendelea kuwemo.

Will Smith akonga nyoyo za mashabiki

MWIGIZAJI Will Smith amekonga kwa aina yake nyoyo za mashabiki wikiendi iliyopita kwa vibao vyake vya zamani akichanganya na vya kisasa.

Will ambaye ni mwanamuziki pia, aliingia kwa kushtukiza katika jukwaa la Ukumbi wa Grammy Museum na kuanza kuimba kwa maudhui ya tamthilia yake ya Fresh Prince of Bel-Air.

Tamthilia hiyo ilifanya vizuri miaka ya 1990 na hivyo nyimbo zake kuwarudisha mbali kihisia mashabiki wake waliokuwepo hapo.

Aidha, Will aliingiwa na huzuni akikumbuka mbali maisha yake ya miaka 32 iliyopita, kwa mara ya kwanza alipoitwa baba kupitia mtoto aliyezaa na mwigizaji, Sheree Zampino.

Baada ya kuzungumza machache jukwaani kuhusiana na hisia hizo, ilidhihirisha kuwa msanii huyo bado anayakumbuka na kuyahitaji maisha yake ya zamani, tofati na sasa akionekana kwenye migogoro ya mara kwa mara na mkewe, Jada Pinkett.

Kanye West aibua maswali Tokyo

INAELEZWA kuwa inatimia wiki ya pili sasa Kanye West anaonekana peke yake bila ya mwenza wake, Bianca Censori.

Rapa huyo juzi ameingia mara mbili kwenye mgahawa wa Jamaica, akionekana kufurahia chakula chao huku akisaini katika ukuta wa mgahawa huo akiwa na furaha.

Hata hivyo, maswali mengi ni yuko wapi mkewe, mbunifu na mwanamitindo, Bianca Censori ambaye amekuwa akizunguka naye sehemu mbalimbali hapo awali.

Mara ya mwisho wawili hao wameonekana pamoja Septemba 20, mwaka huu wakifanya manunuzi mitaa ya Tokyo.

Tangu hapo, Kanye amerejea Tokyo mara mbili ikiwemo wiki iliyopita kuhudhuria pambano la mieleka lakini hakuwa na Bianca. Hakuna fununu za ugomvi baina yao lakini hali hiyo haijazoeleka kwa wawili hao.

 

 

 

Related Articles

Back to top button