Afrika Mashariki

Gor Mahia yaahidi ushindi dhidi ya APR mechi ya ufunguzi CECAFA Kagame Cup

KIGALI: Kocha mkuu wa Gor Mahia, Charles Akonnor, amesema kikosi chake kiko tayari kuonesha kiwango bora zaidi kitakapokutana na mabingwa wa Rwanda, APR, katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 utakaopigwa Ijumaa.

Akonnor amesema hawajakata tamaa kutokana na kupoteza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rayon Sports, akieleza kuwa matokeo hayo yamewapa nafasi ya kujifunza na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza rasmi kwa mashindano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kabla ya mchezo, kocha huyo raia wa Ghana alisema walifaidika na muda walioupata Kigali kwa ajili ya mazoezi na maandalizi, licha ya kuwa wapinzani wao walikuwa wameanza maandalizi mapema zaidi.

“Ni heshima kuwa hapa. Kigali imekuwa nzuri sana kwetu. Tumepata muda wa kufanya mazoezi na pia kufahamu mazingira. Tumekuwa kwenye wiki ya pili ya maandalizi tangu tulipoanza. Tulicheza dhidi ya Rayon Sports na tukapoteza, lakini ilikuwa sehemu ya kujifunza,” alisema Akonnor.

Kocha huyo pia amepongeza waandaaji wa michuano hiyo kwa kutoa elimu kuhusu mabadiliko mapya ya sheria za mchezo wa soka, akisema mafunzo hayo yamekuwa muhimu kwa timu zote zinazoshiriki ili kujiandaa vizuri.

Akizungumzia mchezo dhidi ya APR, Akonnor alisema anatambua kuwa utakuwa mtihani mkubwa kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini alisisitiza kuwa Gor Mahia imejiandaa kupambana na kuonyesha uwezo wake.

Alisema kikosi chake kimeonesha nidhamu, kujituma na kiwango kizuri cha mazoezi katika siku za maandalizi, hali inayompa matumaini kuwa wachezaji wake wako tayari kwa changamoto hiyo.

“Tunaamini katika maandalizi yetu. Ni changamoto kujiandaa kwa msimu mpya huku pia ukishiriki mashindano makubwa kama haya, lakini tunafahamu umuhimu wa mashindano haya na tutajaribu kuonyesha uwezo wetu,” alisema.

Akonnor aliongeza kuwa lengo lao la kwanza si kuzungumzia ushindi pekee, bali ni kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi kuliko mchezo uliopita na kurekebisha makosa waliyoyaona.

“Hatuzungumzi tu kuhusu kushinda, tunataka kufanya vizuri zaidi. Kuna maeneo ambayo tumeyaona yanahitaji kuboreshwa. Tukifanikiwa kuyarekebisha, nafasi yetu ya kupata matokeo mazuri itaongezeka,” alisema.

Gor Mahia na APR zinatarajiwa kutoa ushindani mkali katika mchezo huo wa kwanza wa CECAFA Kagame Cup, huku kila timu ikisaka kuanza mashindano kwa matokeo chanya.

Related Articles

Back to top button