Tetesi

Gamondi, Yanga iko hivi.

ZANZIBAR. BAADA ya mkataba wake kutamatika jana, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amewaaga mashabiki wa timu hiyo kwa kuwa hatarajii kuendelea kuwepo licha ya timu hiyo kutaka huduma yake, huenda akatimkia katika kikosi cha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, baada ya kuonekana kuihitaji huduma yake.

Gamondi aliwaaga mashabiki wa Yanga baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga walitwaa kombe hilo kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya kumaliza dakika 120 kwa suluhu.

Baada ya mchezo huo, Gamondi amesema ilikuwa mechi ngumu lakini anafurahi kuona timu yake imetwaa kombe hilo na amewashukuru benchi zima la ufundi, mashabiki na wachezaji kwa kipindi chote walikuwa wanatafuta matokeo, ushindi wote waliopata maandalizi yake yalianzia mwanzoni mwa msimu.

“Bila maandalizi mazuri tusingepata matokeo mazuri ambayo leo hii yamemfurahisha kila mmoja wetu, nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa wa kutusapoti kila tunapokuwepo,” alisema kocha huyo.

Kuhusu kujiunga na timu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kocha huyo alikiri kuwepo na mazungumzo hayo lakini hakuweka wazi kama ataungana nayo katika msimu ujao au la.

Amesema yeye ni kocha, anaajiriwa lakini anaweza kuondoka na kwenda timu yoyote ambayo anaona ataweza kufanya nayo kazi, hivyo hajui msimu ujao atakuwa wapi huenda akasalia Yanga pia.

“Makocha tunaajiriwa ili kufukuzwa, kama nikiondoka hapa naamini nitapata timu nyingine na nitafanya vizuri na kufukuzwa pia, bila kujali nimeondoka vipi,” amesema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, amekinoa kikosi cha Yanga kwa msimu huu wa 2023/24 na amefanikiwa kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na kuishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).

Ukiacha Kaizer Chiefs, Gamondi amesema amepata ofa kutoka nchi mbalimbali za Afrika hivyo anaamini hata akiondoka Yanga atapata timu nzuri ya kuinoa.

Related Articles

Back to top button