Ligi Kuu

Gamondi: Tabora ni ndogo ila tunawaheshimu

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema licha ya kwamba wanawazidi Tabora United kwa ubora wataingia Uwanjani hapo kesho kwa kuwaheshimu kuhakikisha wanapata pointi tatu.

Akizungumza Dar es Salaam leo kuhusu mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex kesho, Gamondi amesema wanaifahamu Tabora kuwa ni timu ndogo lakini lazima wawaheshmu kwa kuwa wanaweza kuja na mfumo wa kuzuia ili wasifungwe.

“Yanga ndio timu kubwa Tanzania, tunafahamu Tabora ni timu ndogo lakini lazima tuwaheshimu, najua wanaweza kuja na kuzuia zaidi ili tusiwafunge kisha watushambulie kwa kutushtukiza. Tumejiandaa kwa namna yoyote ile watakayokuja nayo, lengo ni pointi tatu.”amesema.

Amesema wamefanya kadiri ya uwezo wao kurejea kwenye ubora na wameshafanya tathmini ya kutosha kubaini ubora wa wapinzani hao, kilichobaki ni kufanyia kazi kutimiza lengo lao la kusalia kileleni mwa ligi.
Gamondi amesema Tabora wamebadilika kimbinu kwani wametoka kushinda mechi mbili za mwisho wakiwa nyumbani. Msimu huu wamefunga magoli tisa lakini wameruhusu magoli 14.

“Nafikiri kocha wao mpya anacheza kwa tahadhari zaidi. Tumejiandaa vyema na ni matumaini yangu tutapata alama tatu muhimu,”amesema.

Kocha wa magolikipa wa Tabora United Khalifan Mbonde amesema amesema wamekuja kupambana, wamejiandaa vizuri ili kupata matokeo.

“Kusudi letu ni tofauti, tumejiandaa japo tumetoka kwenye mchezo mgumu hivi karibuni ila tuko tayari na tunawaheshimu Yanga sana hivyo tumekuja kupambana,”amesema.

Related Articles

Back to top button