Afrika Magharibi

Mchekeshaji MCA Tricky atangaza kuacha utangazaji

NAIROBI: Mchekeshaji na mtangazaji maarufu wa redio nchini Kenya na afrika mashariki, MCA Tricky, ametangaza rasmi kuacha kazi katika kituo cha redio alichokuwa akikifanyia kazi kwa zaidia ya miaka sita.

MCA Tricky, ambaye alijizolea umaarufu kupitia kipindi cha Churchill Show, alitangaza uamuzi huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza kuwa ilikuwa si rahisi kuachana na kituo hicho, lakini ni hatua muhimu kuelekea ukurasa mpya wa maisha yake ya kikazi.

“Nyakati zako ngumu mara nyingi ndizo huzaa mafanikio makubwa zaidi maishani. Tunaendelea kusonga mbele kwa nguvu,” aliandika.

Katika ujumbe mwingine aliouweka kwenye akaunti yake ya Instagram, alisema:
“Safari yangu imefungwa rasmi kwa mafanikio. Asanteni na familia yote.”

Katika kipindi chake cha miaka sita ndani ya kituo hicho, MCA Tricky alikuwa mmoja wa watangazaji waliopendwa zaidi kutokana na ucheshi wake na uwezo wa kuendesha vipindi vilivyowavutia wasikilizaji wengi.

Mbali na kazi ya utangazaji, amejijengea jina kupitia vichekesho vya jukwaani, televisheni pamoja na utengenezaji wa maudhui ya kidijitali, hatua iliyomfanya kuwa miongoni mwa wasanii wenye ushawishi mkubwa nchini Kenya.

Kuondoka kwake kunatajwa kuwa sehemu ya mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya redio nchini Kenya, ambapo watangazaji wengi wamekuwa wakihamia vituo vingine, televisheni, majukwaa ya kidijitali au kuanzisha biashara zao binafsi.

Mashabiki na wadau wa tasnia ya habari na burudani wamepokea kauli hiyo ya Tricky kwa namna tofauti huku wengi wakimpongeza kwa hatua hiyo na kumtakia kila la heri katika safari yake mpya.

Baadhi ya mashabiki wameonyesha imani kuwa tayari anaandaliwa mkataba mpya katika kituo kingine cha redio, ingawa MCA Tricky hajafichua hadharani hatua atakayochukua baada ya kuondoka hapo.
Kwa sasa, hatma ya mtangazaji huyo imeendelea kuwa gumzo mitandaoni, huku mashabiki wakingoja kwa hamu kutangazwa rasmi kwa kituo au mradi mpya atakaojiunga nao.

Related Articles

Back to top button