Nyumbani

Gamondi: Sijali kuhusu yaliyopita, kesho tunaanza upya

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema anafanya mabadiliko kwenye kikosi cha timu yake kuelekea mchezo wa kesho kwa kuwa hakupata nafasi ya kuwaona Simba wakicheza hivi karibuni.

Amesema kesho ni mechi tofauti na kutakuwa na mabadiliko kwa kuwa ni mchezo wa mtoano,atakayepoteza ataondolewa katika mashindano hayo ya Ngao ya Jamii, ambayo nusu fainali hiyo itachezwa kesho, Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Yanga wanashuka dimbani kesho kuwakabili Simba ambayo ina kikosi kipya kuanzia usajili wa wachezaji wapya pamoja na benchi la ufundi tofauti na msimu uliopita ambapo walifanikiwa kuifunga mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Yaliyopita yamepita, sipendelei kufuatilia sana yaliyopita, huu ni msimu mpya hata wapinzani wetu pia wamebadilika kila kitu kimebadilika, wacha tuone kesho kitatokea nini,” amesema kocha Gamondi.

Amesema wapo imara kiakili na kimwili, wamejiandaa vya kutosha na hakuna wanachokihofia japo kuwa hajapata wasaa mzuri wa kuwatazama wapinzani wake kwani mechi nyingi hazikuoneshwa.

“Lakini hiyo sio changamoto kubwa kwani naandaa timu yangu kwa asilimia 75, asilimia 25 ndio natumia kumchunguza mpinzani.  Hakuna siri kwenye mpira kila kitu lazima kiwe hadharani, kesho ni siku muhimu sana kwani ni mechi ya mtoano,” ameeleza kocha huyo.

Amesisitiza kuwa hawapaswi kufanya makosa na wanatakiwa kuwa makini kwenye idara ili kupata matokeo mazuri, naamini mashabiki wao watajitokeza kwa wingi kwa lengo la kuwapa hamasa.

“Kesho ni mchezo wa dabi, hakuna timu ya kawaida (underdog) kwenye mchezo huo kwani ni  maalumu sana. Najua mpinzani wetu ana timu mpya, wachezaji wapya na wote kwa pamoja watachukua fursa hii kuonesha ubora wao. Kimsingi mchezo huu mizani ipo sawa kwa pande zote  yaani 50/50, ni muhimu sana kuendea mchezo huu kwa umakini mkubwa,” amesema.

Kipa wa Yanga Aboubakari Khomein akiwakilisha wachezaji wenzake amesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo wa mtotoano na wanahitaji kuanza vizuri msimu kwa kujituma kupata matokeo ya ushindi.

“Tumejiandaa vizuri sana na tuko tayari, wachezaji wana ari na wote tunawahakikishia kuwa wachezaji tunakwenda kupambana, naamini kesho tutafanya vizuri,” amesema kipa huyo.

Related Articles

Back to top button