Gamondi: Maneno yatawaponza tena
DAR ES SALAAM: Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema amewekeza nguvu zote katika mchezo wa marudiano dhidi ya Vital’o ya Burundi, mchezo utakaopigwa siku ya jumamosi, Agosti 24 jijini Dar es salaam.
Kuelekea katika mchezo huo makocha wa timu hizo, akianza mwenyeji, Miguel Gamondi amesema wanajiamini na matokeo waliyopita lakni wanawaheshimu kwa kuwa wana dakika 90 nyingine za kupambana na kipaumbele chao ni kufuzu hatua inayofuata.
“Huwa sipendi kusikiliza mpinzani anawaza au kuongea nini. Mara nyingi natumia muda wangu kuandaa timu yangu bora. Nina timu bora ambayo imekamilika kila idara. Kwenye mpira ni lazima uwe na weledi kwa kuheshimu wapinzani.
Siwezi kusema kuwa hatuwezi kufungwa goli tano, lakini sio jambo ambalo natarajia kuliona likitokea. Nina matumaini makubwa sana na wachezaji. Nafahamu watakuja kwa nguvu kutafuta magoli, nasi tumejiandaa kwa kila mbinu” amesema Gamondi
Mwakilishi wa wachezaji, Mshery amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na kufuata maelekezo waliyopewa na kocha Gamondi katika uwanja wa Mazoezi.
“Hatutawadharau wapinzani wetu kwa sababu tu tumeshinda mechi ya kwanza, mchezo wa kesho tutaingia kama tunaanza upya mashindano hayo. Lakini pia hamasa ya Goli la Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) inaongeza chachu ya kufanya vizuri zaidi,” amesema Mshery.
Kwa upande wa kocha wa Vital’O, Sahabo Parris amesema mechi ya kwanza walikuwa wanatazama jinsi ya kuwafunga Yanga na walicheza vizuri lakini haikuwa bahati kwao.
Amesema anaimani kubwa na timu yake kufanya vizuri na kuweza kuwapa ushindani mkubwa Yanga zaidi ya mechi iliyopita.
“Nina imani kubwa na wachezaji wangukwa kujiandaa vizuri na ushindi upo, tunaweza kukurudisha mabao 4 na kuwafunga Yanga na kusonga mbele katika mashindano hayo,” amesema Parris.