
TIMU ya Taifa ya Soka ‘Taifa Stars’ imesema inajua namna Uganda The Cranes ilivyo timu
yenye ubora katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwa hivyo wanajiandaa kimbinu kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo dhidi yao utakaochezwa Jumapili.
Mchezo huo wa kwanza wa kufuzu fainali za Mabingwa wa Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana mjini Kampala Septemba 3 na mshindi wa jumla atafuzu fainali zilizopangwa kufanyika Algeria mwakani.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake Kocha Mkuu wa Stars, Kim Paulsen amesema Dar es Salaam kuwa Uganda ni timu imara hawaibezi, bali wanajipanga kulingana na ubora wa wapinzani wao.
“Uganda ni timu nzuri yenye uwezo na kwa kulitambua hilo ni lazima tujipange vizuri kwa kuwaheshimu wapinzani wetu, tunashukuru wachezaji wote wako salama kambini,” alisema.
Alisema kwa siku chache walizoingia kambini wameangalia maeneo yote muhimu kwenye ulinzi namna ya kulinda, namna ya kutengeneza nafasi na kushambulia lengo lao likiwa ni kufanya vizuri.
Kocha wa magolikipa, Muharami Mohamed amesema makipa wake wote watatu wana uwezo isipokuwa anawaongezea mbinu za kuwa bora zaidi.
“Nawajenga kiakili, kiafya na kuongeza vitu vichache vya kiufundi kwa sababu tunakwenda kukutana na mechi ya mashindano ambayo ni ngumu na ya mtoano, ni muhimu kujipanga vizuri pande zote,” alisema.
Alisema kingine amekuwa akizungumza na makipa wake namna ya kujiamini anapokuwa eneo lake la kazi.
Nahodha wa kikosi hicho, Aishi Manula alisema wamejiandaa vizuri na wanaamini utakuwa mchezo wenye ushindani na mgumu kwa kuwa timu hizo zinajuana kwa muda mrefu.
“Tuna imani mwalimu atatuandaa vizuri kulingana na namna alivyowatizama wapinzani wetu,” alisema na kuongeza kuwa ni wakati wao kuonesha uwezo ili kupata matokeo chanya nyumbani na ugenini katika mchezo wa marudiano.