Taifa Stars kurejesha heshima nyumbani
DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa Stars kesho itakuwa kibaruani katika mchezo wa marudiano wa kufuzu Fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Sudan utakaopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Ikumbukwe Taifa Stars wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu za kufungwa bao 1-0 mchezo wa kwanza dhidi ya Sudan, uliochezwa nchini Mauritania.
Kuelekea mchezo wa kesho Kocha wa Stars, Bakari Shime amesema wamejiandaa vizuri na wanafahamu wapo nyuma kwa bao 1-0, wakicheza walivyocheza kama mechi ya kwanza wataibuka na ushindi na kufuzu kwenda kwenye hatua ya mwisho ya mchujo wa tiketi ya CHAN.
“Kiwango tulichokionesha Mauritania wachezaji walicheza kwa ubora hivyo tukihamishia ubora huo katika mchezo huu wa kesho, matumaini yangu mashabiki wataiona Stars mpya zaidi,” amesema.
Shime amesema ameandaa timu kimbinu, kiufundi lakini pamoja na kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia kuondoa dhana ya kutofanya vizuri wanapokuwa uwanja wa nyumbani.
Naye Nahodha wa Taifa Stars, Aishi Manula amesema wapo tayari kwa ajili ya kupambania Taifa lakini michezo hiyo inawapa nafasi ya wachezaji kujitangaza na kutoka.
“Huu mchezo ni muhimu kushinda licha ya kufanikiwa kufuzu kutokana na uwenyeji wetu lakini tunaenda kupeperusha bendera ya Tanzania na tukifanikiwa kuonesha kiwango tulichonesha ugenini watanzania watafurahi,” amesema.
Manula amesema wanaumizwa na dhana iliyopo kuwa hawafanyi vizuri nyumbani kwa kushindwa kutumia Uwanja wa Benjamini Mkapa licha ya kuwa kuna baadhi ya mataifa hujivunia na uwanja wa nyumbani kwa kufanya vizuri.
Mshindi wa mchezo huo atacheza na mshindi wa jumla kati ya Ethiopia na Eritrea, Desemba katika hatua ya mwisho ya mchujo wa tiketi ya CHAN ingawa Tanzania na Kenya zimekwishafuzu kwa tiketi ya uenyeji.