Estadio Azteca na rekodi za kibabe

MEXICO:ESTADIO Azteca, linaweza kuwa jina geni kwa wapenzi wa kandanda wa kizazi cha sasa ila haibadilishi chochote katika uhalisia wa kuwa moja ya viwanja vinavyobeba historia kubwa kupita vyote duniani. Huu ni uwanja wa taifa wa nchi ya Mexico.
Ni uwanja wenye uwezo wa kubeba mashabiki 87,523, idadi inayoufanya kuwa uwanja mkubwa katika ukanda wa Latin America na wa 8 kwa ukubwa duniani.

Dimba la Azteca lilishuhudia Pele akibeba taji lake la mwisho la kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Brazil mwaka 1970 walipoichapa Italia mabao 4-1.Miaka 16 baadaye yaani mwaka 1986, Diego Armando Maradona, gwiji wa soka kutoka Argentina akaiongoza timu yake ya taifa kutwaa kombe la dunia katika uwanja huohuo kwenye mchezo wa kuvutia uliomalizika kwa Argentina kushinda 3-2 dhidi ya Ujerumani.

Licha ya kutumika kama uwanja wa taifa wa Mexico,Uwanja huu haumilikiwi na serikali ya Mexico bali upo chini ya umiliki wa kampuni binafsi ya Televisa.
Dimba hili la kihistoria linashikilia rekodi ya kuwa uwanja pekee kuwahi kufungua michuano ya kombe la dunia mara tatu;mwaka 1970, 1986 na 2026 ambapo mchezo wa ufunguzi utakuwa ni baina ya timu ya taifa ya Africa kusini na timu ya taifa ya Mexico usiku wa leo.




