Eriksen apata nafuu baada ya kuanguka uwanjani

DENMARK: KIUNGO wa zamani wa Manchester United na Tottenham, Christian Eriksen ameanguka uwanjani wakati wa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Denmark na Ukraine uliochezwa mjini Odense juzi Juni 07,2026, hali iliyosababisha mchezo huo kusimamishwa katika dakika ya 65.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Denmark, Eriksen alipoteza fahamu kwa muda mfupi lakini alirejea hali yake ya kawaida haraka na kutembea mwenyewe kutoka uwanjani, hatua iliyowapa afueni mashabiki na wachezaji waliokuwepo uwanjani hapo.
Madaktari wa timu ya taifa ya Denmark wamesema kuwa kifaa maalum cha moyo (ICD) kilichowekwa kwa mchezaji huyo kilifanya kazi kama ilivyokusudiwa, na kilimsaidia kurejesha fahamu kwa haraka baada ya tukio hilo la ghafla.
Eriksen alifungwa kifaa hicho baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa michuano ya Euro 2020 mwaka 2021, tukio lililobadilisha maisha yake ya soka lakini haikumzuia kurejea uwanjani baada ya matibabu na uangalizi maalum.
Daktari wa timu ya taifa ya Denmark, Morten Boesen, amesema Eriksen alikuwa katika hali nzuri baada ya tukio hilo na tayari alikuwa akiwasiliana na wachezaji wenzake akiwa hospitalini, akiwatuma salamu kuwa yuko salama.
Nahodha wa Denmark, Pierre-Emile Højbjerg, amesema tukio hilo liliwatisha sana wachezaji wote uwanjani, lakini amepongeza kasi ya wataalamu wa afya waliotoa msaada wa haraka na wa kitaalamu.
Baada ya tukio hilo, mchezo ulisitishwa rasmi na wachezaji wa timu zote mbili walionekana kusimama kwa umoja kuonesha mshikamano na kumuombea afya njema Eriksen.
Uongozi wa timu ya taifa ya Denmark umesema utaendelea kufuatilia hali ya mchezaji huyo huku uchunguzi zaidi wa kitabibu ukiendelea kubaini chanzo cha tukio hilo.




