Samatta mwili Ulaya, moyo upo Tanzania

DAR ES SALAAM; Baridi ya jioni, ikiambatana na mvua za barafu barani Ulaya humkuta akipambana kwenye viwanja vya kisasa, taa zikimulika kila hatua yake. Ajabu iliyoje ndani ya kifua chake, kuna joto la Bahari ya Hindi, sauti za Mbagala, na ndoto za vijana wa Kitanzania.
Huyo ndiye Mbwana Ally Samatta, nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na mshambuliaji wa Le Havre AC inayoshiriki Ligue 1 ya Ufaransa. Mwili wake unapambana Ulaya, lakini moyo wake unadunda Tanzania.
Kuna nyakati katika historia ya soka, ambapo taifa linahitaji kiongozi si wa kupiga kelele, bali wa kuonesha njia. Samatta amekuwa dira hiyo.
Chini ya unahodha wake, Tanzania imefuzu michuano ya Mataifa Afrika (AFCON) mara tatu 2019 nchini Misri, 2023 Ivory Coast na 2025 nchini Morocco. Kabla yake, ilikuwa ni historia nadra ya kushiriki mara moja tu 1980 nchini Nigeria. Leo ni hadithi ya matumaini.
Kila bao lake limekuwa zaidi ya alama ubaoni. Limekuwa mwaliko wa vijana kuamini kuwa inawezekana. Limekuwa ushahidi kuwa nidhamu, kujitoa na uzalendo huzaa matunda.

Safari yake ilikuwaje kutoka kwao Mbagala hadi kuwika Afrika na Ulaya?
Safari yake ilianzia Mbagala Market kabla ya kuonwa na rada za mnyama Mnyama Simba SC ya Kariakoo, akijifunza na kuelewa maana ya kupigania nembo. Akaivuka mipaka, akatua TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako aligeuka kuwa tishio la walinzi na shujaa wa mashabiki.
Msimu wa 2015-2016Akiwa Mazembe, Samatta alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa wanaocheza ligi za ndani heshima iliyompa hadhi ya kifalme barani.
Ulaya ikavuta pumzi. KRC Genk wakamvua Afrika kwa upole wa ndoano. Ubelgiji ukaimba jina lake. Mabao yake yakawa muziki wa viwanjani.
Ndoto zikazidi kukua. Mlango wa Premier League ukafunguka kupitia Aston Villa FC. Tanzania ikafurika mtandaoni, fahari ikipepea kama bendera.
Lakini Samatta si mfungaji wa mabao pekee ni mshindi wa ndoto na mpambanaji wa matumaini ya wale wasio na nguvu wala sauti.
Si nia yangu kuzungumzia historia ya nguli huyo katika soka, ndiyo sababu sitagusia mafanikio yake katika klabu nyingine alizopita kama vile K.R.C ya Ubelgiji, Fernabahce ya nchini Uturuki, PAOK ya Ugiriki, bali ni jambo linalotaka kufanyika Machi 6, 2026.
Ni jambo gani hilo? Hilo ndiyo lililobeba neno moyo upo Tanzania! Kwani siku hiyo saa 10 alasiri Samatta anatarajiwa kuzindua Kituo cha Kulelea Yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu nyumbani kwao Mbagala Majimatitu, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam. Mradi utakaotoa makazi, malezi, elimu na mwanga wa kesho kwa watoto wanaohitaji mkono wa msaada.
Kwa Samatta, ushindi si kelele za mashabiki. Ni tabasamu la mtoto anayepata kitanda salama cha kulala. Ni ndoto ya mtoto inayolindwa dhidi ya giza la umaskini.
Hatua yake inaendana na nyota wengine wa Afrika kama Sadio Mané, ambaye amewekeza katika shule na hospitali nchini Senegal. Wote wanafundisha somo moja: umaarufu una thamani pale unapogeuzwa kuwa daraja la matumaini.
Miaka yake Ulaya imemjenga kama mchezaji. Lakini moyo wake Tanzania unamjenga kama kiongozi.
Kupitia mradi huu, Samatta haandiki tu historia ya mabao, bali historia ya kuigusa jamii. Haachi tu alama kwenye nyasi za viwanja vya Ulaya, bali anaacha alama kwenye mioyo ya watoto wa Tanzania. Mwili wake upo Ulaya. Lakini moyo wake uko Tanzania.




