Eder Militao ahofiwa kukosa mechi kadhaa

MADRID: WABABE wa soka la Ulaya Real Madrid wamethibitisha kwamba beki wao raia wa Brazil, Eder Militao, amepata majeraha ya nyonga, ingawa klabu hiyo haijaweka wazi muda atakaokaa nje ya uwanja.
Katika taarifa yao ya Jumatano, Madrid imesema vipimo vilivyofanywa na timu ya madaktari vimeonesha kwamba Militao ana jeraha la misuli katika eneo la nyonga, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu ukali wake.
Militao alihisi maumivu makali dakika ya 58 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Brazil na Tunisia mjini Lille nchini Ufaransa, uliomalizika kwa sare ya 1-1, na alilazimika kuomba kutolewa nje.
Vyombo vya habari nchini Hispania vimeripoti kuwa beki huyo huenda akawa nje kwa takribani wiki mbili, hali ambayo inaweza kumfanya kukosa mechi ya LaLiga dhidi ya Elche Jumapili hii, safari ya wiki ijayo kwenda Girona, pamoja na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Olympiacos Jumatano ijayo.




