Muziki

Diddy atengwa na wafungwa wenzake

NEW JERSEY: GEREZA la FCI Fort Dix limeripotiwa kumrejesha rapa P. Diddy katika Kitengo Maalumu cha Makazi, kinachojulikana kama kifungo cha upweke.

Vyanzo mbalimbali vimeuambia Mtandao wa TMZ kuwa Diddy amerudishwa huko kufuatia ripoti ya NBC News kuhusu madai ya kuishi maisha ya kifahari gerezani.

Maisha hayo yanajumuisha huduma za ‘masaji’, milo ya gharama, pombe zilizopigwa marufuku, wafungwa wenzake kufanya kazi zake za kila siku pamoja na video iliyovuja juzi ikimuonesha akitumia simu gerezani kinyume cha sheria.

Uongozi wa Fort Dix umechukua uamuzi wa kumtenga Diddy, ikidaiwa ni utaratibu wa kawaida wakati maofisa wa gereza wakifanya uchunguzi juu ya shutuma hizo.

Hii si mara ya kwanza Diddy kuwekwa kwenye kifungo cha upweke kwani Julai, mwaka huu aliwekwa huko baada ya kuhusika katika ugomvi gerezani.

NBC ilienda mbali na kuripoti wafungwa wengine walisafisha choo chake kabla ya yeye kukitumia, kumtandikia kitanda, kumfulia nguo na kumpikia vyakula kama kuku na pizza.

Imefafanuliwa watu wa karibu na Diddy wamedaiwa kuweka maelfu ya pesa kwenye akaunti zao za duka la gereza ambazo zinatumika kulipia huduma hizo.

Kulingana na rekodi za Ofisi ya Shirikisho ya Magereza, Diddy kwa sasa anatarajiwa kuachiwa huru Januari 21, 2028, tarehe ambayo imebadilishwa mara kadhaa baada ya awali kupangwa kuwa Juni, 2028.

Diddy alihukumiwa mwaka 2025 kwa mashtaka mawili ya kusafirisha watu kati ya majimbo kwa ajili ya ukahaba na kuhukumiwa kifungo cha miezi 50.

Related Articles

Back to top button