Jeanine mambo safi China

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga Princess, Jeanine Mukandayisenga, amezidi kung’ara katika soka la China baada ya kufikisha mabao matatu akiwa na klabu yake ya Wuhan Jiangda WFC.
Jeanine, ambaye ni raia wa Rwanda, ameendelea kuonesha makali yake katika Ligi Kuu ya Wanawake China, akitumia uwezo wake wa kufumania nyavu kuisaidia timu yake katika mbio za ushindani wa ligi hiyo.
Mshambuliaji huyo amefunga bao katika ushindi wa Wuhan Jiangda wa mabao 3-2 dhidi ya Shanghai RCB, jana, akiongeza idadi ya mabao yake katika ligi hiyo hadi matatu.
Kabla ya kuhamia China, Jeanine alikuwa akikipa makali kikosi cha Yanga Princess, ambacho alikihudumia kwa mafanikio na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu wa 2025/2026 kwa mabao 20.
Mafanikio hayo yalikuwa sehemu ya safari yake ya soka inayomfikisha katika hatua nyingine ya kucheza ligi ya kimataifa, baada ya awali pia kufanya vizuri nchini Rwanda akiwa na Rayon Sports.




