Msuva, Mabula waita Watanzania kuwasapoti

ZANZIBAR: MSHAMBULIAJI i wa Taifa Stars, Simon Msuva, amewataka Watanzania na Wazanzibari kujitokeza kwa wingi kesho katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kuishangilia timu hiyo itakapovaana na Nigeria katika mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Msuva amesema kikosi kimewasili salama Zanzibar na wachezaji wote wako katika hali nzuri kiafya, huku maandalizi yakiendelea vizuri kuelekea mchezo huo wa marudiano baada ya kupoteza kwa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza nchini Nigeria.
“Tumefika salama Zanzibar na tunamshukuru Mungu wote tuko wazima. Tuna mchezo mwingine dhidi ya Nigeria na tunacheza nyumbani, naamini mchezo utakuwa mzuri,” amesema Msuva.
Amesema Watanzania na Wazanzibari wana upendo mkubwa kwa soka na wamekuwa wakitoa sapoti kwa Taifa Stars, hivyo anaamini safari hii watajitokeza kwa wingi zaidi kuliko mchezo uliopita.
Ameongeza kuwa ushindi dhidi ya Nigeria utakuwa na manufaa kwa wachezaji, timu ya Taifa na Tanzania kwa ujumla, ikiwamo kuboresha nafasi ya nchi katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kwa upande wake, Alphonce Mabula baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, wanahitaji sapoti kubwa ya Watanzania na Wazanzibari watakaofika Uwanja wa Amaan ili kuwapa nguvu ya kupambana kutafuta matokeo mazuri.
“Tunaomba sapoti ya Watanzania wote, hasa Wazanzibari, waje kwa wingi Uwanja wa Amaan kutusapoti. Nadhani nguvu yao itatupa hamasa ya kufanya vizuri na kupata matokeo mazuri zaidi,” amesema.
Mchezo huo wa marudiano dhidi ya Nigeria utapigwa kesho, Novemba 17, katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kuanzia saa 10:00 jioni




