Africa

Ngorongoro heroes kulipa kisasi kwa Misri?

CAIRO: TIMU ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inatarajia kushuka dimbani kuvaana na wenyeji Misri katika mchezo wa pili wa kirafiki utakaopigwa saa 12 jioni kwa saa za Tanzania, ikiwa na dhamira ya kuonesha kiwango bora zaidi baada ya mchezo wa kwanza.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Mario Rivera, kinakutana tena na Misri baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0 Novemba 12, mwaka huu.

Rivera amesema maandalizi yao yamejikita zaidi katika kukijenga kikosi, kuwafahamu vizuri wachezaji na kuendeleza mfumo wa uchezaji anaoutaka, huku akisisitiza kuwa mchezo wa pili unatarajiwa kuwa bora kutokana na wachezaji kupata uelewa na kujiamini zaidi.

“Tunajikita zaidi katika timu yetu. Lengo kubwa la maandalizi ni kuwafahamu wachezaji na kuendeleza mfumo wetu wa uchezaji. Tunataka kufanya mambo yetu vizuri zaidi na kuboresha kiwango tulichoonesha kwenye mchezo uliopita,” amesema Rivera.

Ameongeza kuwa mchezo wa kwanza ulikuwa muhimu kwa kuwapa wachezaji wengi nafasi ya kuonesha uwezo wao, hivyo anaamini uzoefu walioupata utawasaidia kuingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na ujasiri mkubwa na ari ya kuonyesha zaidi kile walichonacho.

Kocha huyo amesema ingawa kuna baadhi ya mambo wanapaswa kuyazingatia kulingana na aina ya uchezaji wa wapinzani, kipaumbele chao kikubwa ni kuboresha utendaji wa timu yao na kutekeleza falsafa ya uchezaji wanayoijenga.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya Ngorongoro Heroes kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa, huku benchi la ufundi likitumia nafasi hiyo kupima uwezo wa wachezaji na kujenga kikosi chenye ushindani.

Related Articles

Back to top button