Marioo: Bongo Fleva bado haijulikani duniani

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI Marioo ameeleza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuupeleka muziki wa Bongo Fleva kusikika Marekani, Ulaya na kwingineko.
Marioo amefunguka hayo alipokuwa akizungumzia matokeo ya safari ya ziara yake ya muziki iliyomfanya akae Marekani kwa takriban kipindi cha mwezi mmoja.
“Kwa upande wa promota mwenyewe anasema hii ziara ilikuwa nzuri sana kwa upande wake na hata kwetu pia ilikwenda vizuri kabisa, na namna gani watu wamepokea vizuri hii kitu, Novemba narudi tena kupiga shoo kwenye majimbo mawili.
“Lakini kiujumla kimuziki kusema ukweli, ‘game’ yetu Bongo Fleva bado haijapita duniani.
“Makak wamejitahidi kufanya kwa sehemu yao lakini sisi vijana sasa inabidi kuchukua hilo jukumu, tuisukume zaidi, waliopambana ni vizuri lakini inabidi tuweke nguvu zaidi,” alisema Marioo.
Akitolea mfano wake yeye binafsi, amedai tangu amekwenda Marekani hajasikia wimbo wa Bongo Fleva hata mmoja.
Amefafanua kuwa nyimbo hizo zinasikika tu pale kwenye ukumbi kunapokuwa na DJ mzawa kutoka Tanzania ndio husikika ngoma za Bongo Fleva kwa kiasi, lakini tofauti na hapo ni ngumu kuzisikia.
Akizungumzia jitihada za wasanii wengine kuufikisha mbali muziki huo, amesifia kwa upambanaji wao mkubwa lakini akasisitiza bado kunahitajika nguvu kubwa kuupeleka mbali muziki huo.




