Muziki

Quavo aeleza alivyomaliza bifu na Offset

NEW YORK: RAPA Quavo ameweka wazi kuwa bifu lake na rapa Offset lilimalizika punde baada ya kifo cha Takeoff kilichojiri mwaka 2022.

Quavo ameeleza hayo alipokuwa akihojiwa na podcast ya Idea Generation ya Mtandao wa Complex na kufunguka kwamba hakuona tena sababu ya chuki baina yao baada ya kifo cha mwenzao huyo ambao pamoja walikuwa wakiunda Kundi la Migos.

Takeoff aliuawa Novemba Mosi, mwaka 2022 kwa kupigwa risasi huko Houston, Texas na mpaka sasa kesi ya tukio hilo inaendelea kuunguruma mahakamani.

Quavo amesema baada ya tukio hilo, mambo yaliyokuwa yakimkasirisha kuhusu Offset hayakuwa tena na umuhimu kwake na hakuona faida ya kuendelea nayo moyoni.

“Nikizungumza kwa upande wangu, sikuina tena kama kuna faida ya kuendelea kurumbana au kumkasirikia Offset, nilichokuwa napitia naamini ndicho alichokuwa akipitia kwa hiyo sikuona maana ya hasira dhidi yake,” alisema Quavo.

Jumapili iliyopita, wawili hao walionekana pamoja jijini Los Angeles, wakitambulisha wimbo wao mpya wa Away ambao ni kolabo yao ya kwanza tangu mwaka 2022.

Away ni wimbo unaopatikana kwenye albamu mpya ya Quavo, Qrömelife inayotarajiwa kuachiwa Oktoba 2, mwaka huu.

Taarifa zaidi ni kuwa, marapa hao wamethibitisha kurejea kwa Kundi la Migos na wanaipika albamu yao ya mwisho wakiwa pamoja.

Wakati huohuo, Quavo alieleza furaha aliyonayo kwa kupata mtoto wa kike akibainisha hilo limempa nguvu, ari, furaha na ujasiri mpya katika mapambano ya kimaisha.

Lakini mpaka sasa hijawekwa wazi jina la binti yake huyo wala utambulisho wa mwanamke aliyepata naye mtoto huyo.

 

Related Articles

Back to top button