Bushoke afunguka safari ya Marekani

MSANII wa muziki, Lutha Bushoke, amesema kwa sasa yupo nchini Marekani, ambako amefika kwa mwaliko wa Joseph Chameleon kwa ajili ya kazi.
Bushoke amesema urafiki wao wa muda mrefu umezaa matunda na anapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Kamilioni.
“Nipo naye hapa Boston, Marekani. Yeye ndiye amenialika mpaka hapa nilipo, kila kitu ni yeye, hata hii connection mpaka hii interview tunayofanya sasa hivi, yeye yupo nyuma,” amesema Bushoke.
Bushoke amemshukuru Chameleon kwa upendo wake, akisema wamekuwa marafiki kwa takriban miaka 20.
Kuhusu afya ya Chameleon, Bushoke amewatoa wasiwasi mashabiki kwa kusema anaendelea vizuri.
“Anawashukuru sana mashabiki wake kwa kumuombea dua. Anajua watu wengi wanampenda na hata mimi nilipokuwa nikitembea, watu wengi sana walikuwa wakiniuliza kwa huzuni, ‘bana vipi Chameleon rafiki yako anaendeleaje?’ Nikawaambia anaendelea vizuri.
Lakini sasa hivi kupitia nafasi hii, nawaambia Chameleon anaendelea vizuri sana na anawasalimia wote. Hivi karibuni, Mungu akipenda, mtamuona na atasalimiana na mashabiki wake mwenyewe.”
Bushoke pia ametangaza ujio wa wimbo wake mpya unaoitwa “Mwana Gwe”, ambapo amemshirikisha Weasel Manizo, mdogo wake Chameleon.
Katika hatua nyingine, Bushoke amesema amefungua akaunti mpya ya Instagram kwa jina la Bushoke, na kuwaomba mashabiki wake wamfuate huko.