Kwingineko

Hoja za mwisho zaanza katika kesi ya kifo cha Maradona

BUENOS AIRES, Argentina: WAENDESHA mashtaka nchini Argentina wameanza kutoa hoja zao za mwisho katika kesi inayohusu kifo cha gwiji wa soka duniani, Diego Maradona, wakidai kuwa timu ya madaktari iliyokuwa ikimhudumia ilimtelekeza na kumwacha katika hali iliyohatarisha maisha yake.

Kesi hiyo inayowakabili wataalamu saba wa afya, akiwemo daktari wake mkuu, daktari wa magonjwa ya akili, mwanasaikolojia na wauguzi, ilianza kusikilizwa Aprili mwaka huu.

Maradona alifariki Novemba 25, 2020, akiwa na umri wa miaka 60, takribani wiki mbili baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa donge la damu kwenye ubongo.

Gwiji huyo aliyekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Argentina kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 1986 alifariki kutokana na moyo kushindwa kufanya kazi na hali ya majimaji kujikusanya kwenye mapafu. Wakati huo alikuwa akipatiwa huduma za kupona nyumbani katika eneo la Tigre, pembezoni mwa jiji la Buenos Aires.

Katika hoja zake za mwisho, mwendesha mashtaka Patricio Ferrai alisema mpangilio usioridhisha wa huduma za matibabu ulimweka Maradona katika mazingira ya kutokuwa na msaada, akidai kuwa wahudumu hao walishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Washtakiwa wanakabiliwa na tuhuma za kutambua uwezekano wa matendo yao kusababisha madhara makubwa lakini kuendelea na mwenendo huo.

Upande wa mashtaka pia umehoji uamuzi wa kumruhusu Maradona kuendelea kuuguza afya yake nyumbani badala ya hospitalini. Ulitaja ukosefu wa vifaa muhimu, ikiwemo kitanda maalumu cha hospitali, mashine ya kumsaidia mgonjwa kurejesha mapigo ya moyo na upatikanaji wa haraka wa gari la wagonjwa, kuwa ni sehemu ya ushahidi wa uzembe unaodaiwa.

Wataalamu wa afya walioitwa kutoa ushahidi walisema dalili kama kuvimba mwili, mapigo ya moyo kwenda kasi na shida ya kupumua zilipaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Hata hivyo, wataalamu hao wa afya wamekanusha mashtaka dhidi yao, wakisisitiza kuwa kifo cha Maradona hakikuweza kutabiriwa na kwamba kila mmoja alitekeleza wajibu wake. Iwapo watapatikana na hatia, wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 jela. Hoja za mwisho zinatarajiwa kuchukua takribani wiki mbili kabla ya mahakama kutoa hukumu katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

Kesi ya kwanza kuhusu kifo cha Maradona ilifutwa mwaka jana baada ya kufichuka kuwa mmoja wa majaji alihusika kwa siri katika utayarishaji wa filamu ya makala kuhusu kesi hiyo. Tukio hilo lilisababisha mchakato mpya wa kisheria kuanza.

Related Articles

Back to top button