Colman Domingo afunguka urafiki wake na Chadwick Boseman

NEW YORK: MUIGIZAJI maarufu wa Hollywood, Colman Domingo, amefunguka kuhusu uhusiano wake wa karibu na marehemu Chadwick Boseman, akieleza jinsi nyota huyo wa filamu ya Black Panther alivyokuwa chanzo kikubwa cha hamasa na mwongozo katika maisha yake ya kisanii.
Domingo, ambaye alicheza pamoja na Boseman katika filamu ya ‘Ma Rainey’s Black Bottom’ ya mwaka 2020, alisema kuwa licha ya kifo cha mwigizaji huyo, bado anahisi uwepo wake na ushawishi wake katika maisha ya watu wengi waliowahi kufanya kazi naye.

Akizungumza katika mahojiano, Domingo alimwelezea Boseman kama rafiki wa kipekee ambaye alikuwa tayari kuwainua wengine katika tasnia ya filamu. Alisema Boseman alikuwa miongoni mwa watu wachache walioweza kuelewa changamoto za waigizaji Weusi nchini Marekani na mara nyingi alikuwa tayari kutoa ushauri kuhusu namna ya kujitetea na kusaidia wengine katika safari ya mafanikio.
Domingo alikumbuka tukio moja lililotokea baada ya mafanikio makubwa ya filamu ya Black Panther mwaka 2018. Alisema alimkuta Boseman akiwa amezungukwa na watu wengi wa tasnia ya filamu katika hafla moja ya Hollywood na akaenda kumpongeza kwa mafanikio yake.
Badala ya kuzungumzia mafanikio yake mwenyewe, Boseman aliwatambulisha watu waliokuwapo kwa kumuelezea Domingo kama mwigizaji mwenye kipaji kikubwa na kuwaambia wafuatilie kazi zake.
Kwa mujibu wa Domingo, kitendo hicho kilimgusa sana kwa sababu kilionesha unyenyekevu na moyo wa kusaidia wengine ambao Boseman alikuwa nao hata wakati alipokuwa katika kileleni cha mafanikio yake.
Hata hivyo alisema anaamini urithi wa Boseman utaendelea kuishi kupitia kazi zake, maneno yake ya kutia moyo na mchango wake kwa kizazi kipya cha waigizaji.
Boseman, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 43 kutokana na saratani ya utumbo mpana, anakumbukwa kwa filamu mbalimbali zilizompatia sifa duniani, ikiwemo ‘Black Panther’, ‘42’, ‘Marshall’ na ‘Da 5 Bloods’. Hadi leo, waigizaji wengi wa Hollywood wanaendelea kumtaja kama mmoja wa watu waliowahamasisha kufikia mafanikio katika tasnia ya filamu.



