BurudaniFilamu

BECKETT: Kila hatua inaashiria kukisogelea kifo

MCHANA wa siku hii umekuwa mzuri sana kwa wapendanao, watalii toka nchini Marekani, na kila mmoja anafurahia sana uhusiano wao.

Ni wakati huu ambao wapenzi hawa, Beckett na April, wapo matembezini nchini Ugiriki.
Lakini usiku wa siku hii ukaenda kuwa mbaya sana kwani giza linapoingia tu linakatisha uhusiano wao. Kufumba na kufumbua April hakuwa anahema tena mbele ya mpenzi wake Beckett.

Hii inatokea wakati wakijaribu kuondoka jijini Athens ili kukwepa machafuko ya kisiasa yanayoendelea, na wakiwa ndani ya gari wakielekea sehemu ya kupumzika iliyo umbali
mrefu kutoka mahali walipo, Beckett aliye kwenye usukani anasinzia na kushindwa kuumudu usukani, hatimaye gari linapinduka na kugonga nyumba moja isiyokaliwa na mtu.

Katika sakata hilo Beckett anamwona mvulana mdogo akiondolewa haraka eneo hilo na mwanamama mmoja mwenye nywele za blonde. Kisha anapoteza fahamu na anakuja kuzinduka na kujiona yupo hospitali.

Siku inayofuata anapelekwa katika kituo cha polisi na maofisa wa Ugiriki, huko anatoa maelezo yake mbele ya ofisa wa polisi, Xenakis, kuhusu ajali hiyo lakini anajikuta akifanya kosa kubwa kwa kusema kwamba ndani ya nyumba aliyoigonga alimwona mvulana mdogo.

Ndiyo… hilo linakuwa kosa kubwa! Pasipo kujua kwamba kauli yake inaweza kuyagharimu maisha yake yaliyonusurika kwenye ajali, Beckett anajikuta akianza kuwindwa kama digidigi.

Kizaazaa kinaanzia hapo kwani kitendo cha kusema kwamba alimwona mvulana
mdogo ndani ya nyumba ambayo inaaminika kutelekezwa na kutokaliwa na mtu kinamfanya atafutwe kila kona, tena kwa siri sana, na maofisa wa polisi pamoja na
wauaji wa kukodiwa.

Nia yao ni kujaribu kuficha ushahidi kwa sababu mvulana huyo mdogo ni mtoto wa mwanasiasa mkubwa nchini Ugiriki, Karras (Yorgos Pirpassopoulos), kiongozi aliyechaguliwa hivi karibuni ambaye anasemekana kuwa na ushawishi mkubwa nchini humo.

Mtoto huyo ametekwa na hajulikani alipo kitendo kina chodhaniwa kuwa kutekwa kwake kutammaliza nguvu Karras, na sasa Beckett anaibuka na ndiye mtu pekee anayefahamu ni wapi alipo mvulana huyo mdogo.

Beckett anatoroka na sasa maisha yake yanakuwa ya kutangatanga kama digidigi, mtu mweusi aliyejitokeza kama kidole gumba katika viunga vya Athens na badala yake anakuja kugundua kuna mchezo mchafu kwa sababu ya siasa.

Ni wakati huu ambao anaomba msaada wa kufikishwa ubalozi wa Marekani kisha anakutana na wanaharakati wawili, Eleni (Maria Votti) na Lena (Vicky Krieps) wakati wanabandika picha za mvulana mdogo aliyetoweka.

Beckett anamtambua kuwa ndiye aliyemwona katika nyumba aliyoigonga. Wanaharakati hawa wanamweleza kuwa huyo mtoto anaitwa Dimos Karras, ni mtoto wa mwanasiasa
Karras aliyetekwa na watu wasiojulikana.

Beckett sasa anaungana na wanaharakati Eleni na Lena, kisha wanasafiri pamoja kwenda mjini Athens huku akilazimika kukwepa mitego. Jambo ambalo hakulijua ni kwamba kila hatua anayoipiga anajikuta akiingia kwenye mlolongo wa matukio ya hatari yanayomfanya
kukikaribia kifo chake mwenyewe na sasa hatakiwi kumwamini yeyote.

Kuna wakati anambana polisi na maofisa wa ubalozi wake wa Marekani wanaoonesha kutaka kumgeuka. Sasa analazimika kukabiliana na kila aina ya hila zinazomkabili. Huko Athens maandamano ya kisiasa yanazuka na haieleweki kama yana uhusiano wowote na Karras ambaye anasemekana kuwa na rekodi fulani chafu.

Wakati huu kuna vitendo vingi vya unyanyasaji dhidi ya watu masikini, na kwamba Karras anamiliki shirika la siri la uhalifu na utakatishaji fedha. Hata hivyo, machafuko hayo ya
kisiasa hayamwachi salama Karras, anauawa.

Katika harakati za kujinasua kutoka kwenye sakata hilo Beckett anajionya kwamba “vitu vingi haviko kama inavyoonekana kwa macho,” na sasa anajikuta akipambana kufa na kupona, anajeruhiwa kwa kisu, anadungwa kisu na hata kupigwa risasi (tena na tena).

Katika kilele cha stori hii na wakati wa kufurahisha zaidi, Beckett anaruka toka ghorofa kadhaa za jengo na kutua kwenye paa la gari linaloondoka toka kwenye maegesho, ndani ya gari hilo yumo mtekaji akiwa na mtoto Dimos Karras.

Kuna mengi ya kusisimua ndani ya filamu hii, itafute uitazame hakika hutojutia. Ni bonge moja la stori. Kupitia mauaji yote yanayotokea, filamu ya Beckett bado inabakia kuwa kitendawili kweli kweli!

Filamu hii ya dakika 108 haikupata mapokezi mazuri toka kwa wakosoaji wa filamu ambao wameipa alama 5 kati ya 10 na wastani wa asilimia 48. Oktoba 2020, mtandao wa Netflix ulipata haki za usambazaji wa filamu hii, wakati huo ikiwa imepewa jina la ‘Born to Be Murdered’, na ikapangwa kutolewa rasmi mwaka 2021.

Januari 2021, ilitangazwa kuwa filamu hii imebadilishwa jina na sasa itaitwa Beckett.
Ilioneshwa kwa mara ya kwanza katika Tamasha la 74 la Filamu la Locarno mnamo Agosti 4, 2021 kabla ya kuachiwa rasmi mnamo Agosti 13, 2021 kwenye mtandao wa Netflix. Ni filamu ya Marekani lakini picha zake zimepigwa katika nchi za Italia na Ugiriki.

Sms: 0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

Related Articles

Back to top button