Muziki

Chief Godlove aweka rehani mali zake kisa msanii wake mpya

DAR ES SALAAM: MSANII na mfanyabiashara maarufu, Godlove Mwakibete ‘Chief Godlove’, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kuweka wazi azma yake kuhusu mafanikio ya msanii wake mpya wa kike.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chief Godlove amesema kuwa yuko tayari kugawa mali zake zote kwa watu wasiojiweza endapo msanii huyo hatapata mafanikio makubwa, ikiwemo kufika katika soko la kimataifa.

“Kama huyu mwanamuziki hataenda kimataifa na hatofanya vizuri, basi mali zangu zote nitagawa kwa maskini na nitarudi shambani kulima,” ameandika Chief Godlove.

Aidha, ameeleza kuwa msanii huyo anatoka katika familia ya kawaida, na dhamira yake ni kumuunga mkono ili aweze kufikia ndoto zake.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya msanii huyo hayategemei juhudi zake pekee bali pia mchango wa Watanzania kwa ujumla.

Chief Godlove pia aligusia changamoto zilizokuwepo zamani kwenye tasnia ya muziki, akieleza kuwa kulikuwa na ushindani usio na afya ambapo ili msanii mmoja apande, mwingine alilazimika kushuka.

Hata hivyo, amesema kizazi cha sasa kinapaswa kubadilika na kushirikiana zaidi.

“Huyu si mwanamuziki wangu tu, ni mwanamuziki wa Watanzania. Mimi nitamsapoti, lakini nyie ndio mtaamua,” ameongeza.

Kauli yake imezua gumzo miongoni mwa wadau wa muziki, wengi wakijiuliza ni nani hasa msanii huyo mpya anayetarajiwa kuletwa kwenye tasnia huku wengine wakihisi ni Rubby wengine wakisema ni Lulu Diva.

Related Articles

Back to top button