CAF yashusha rungu Yanga

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeipiga faini ya dola za Marekani 5,000 (Sh milioni 11) klabu ya Yanga kutokana na Rivers United ya Nigeria kulalamika kufanyiwa vurugu walipokuja kucheza mwezi uliopita mchezo wa kwanza wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Timu hizo zilipambana katika uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0
Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa, mechi hiyo iliyopaswa kuchezwa bila mashabiki, ilionekana kuhudhuriwa na baadhi ya mashabiki.
Baada ya mchezo huo, Rivers ililalamika kupitia mitandao ya kijamii kuwa ilifanyiwa vurugu ikiwamo kupigwa kwa Ofisa Habari wake, Charles Mayuku.
“Yanga ilipata taarifa ya malalamiko ya Rivers United pamoja na uamuzi wa CAF kupitia TFF lakini haikujibu chochote,” ilisomeka taarifa hiyo ya TFF iliyosainiwa na Ofisa Habari wake, Cliford Ndimbo.
Pia, Tanzania ilipewa onyo kutokana na kuripotiwa kwa matukio mbalimbali kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na masuala ya vipimo vya Covid-19.
“Tanzania imetakiwa kuheshimu na kufuata kanuni, taratibu na maelekezo ya Caf,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TFF, kutokana na tukio hilo ilikutana na timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa ili kufanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza katika michezo ya awali.
Timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa ni Simba (Ligi ya Mabingwa Afrika), Azam na Biashara United (Kombe la Shirikisho Afrika.)