Bodi ya filamu yazindua filamu “Kifurushi” kuelimisha jamii dhidi ya dawa za kulevya

DAR ES SALAAM:BODI ya Filamu Tanzania imezindua filamu ya “Kifurushi” inayolenga kuelimisha jamii kuhusu athari za usafirishaji wa dawa za kulevya na umuhimu wa kuzingatia taratibu sahihi za usafirishaji wa mizigo.
Uzinduzi huo, uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Filamu hiyo imeandaliwa na DCEA kwa uratibu wa Bodi ya Filamu Tanzania ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuelimisha umma kuhusu madhara ya biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, amesema filamu ni nyenzo muhimu ya mawasiliano inayoweza kufikisha ujumbe kwa ufanisi na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika jamii.
Dkt. Kasiga amepongeza hatua ya DCEA kutumia sanaa ya filamu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kuzihimiza taasisi za umma na binafsi kutumia filamu kama chombo cha kuelimisha jamii na kuhamasisha maendeleo.
Aidha, amesema Bodi ya Filamu Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha filamu zinatumika kuwasilisha ujumbe wenye manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali Lyimo ameishukuru Bodi ya Filamu Tanzania kwa kuratibu utayarishaji wa filamu hiyo na kueleza kuwa itaoneshwa katika mabasi yaendayo mikoani ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza uelewa kuhusu hatari za dawa za kulevya.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji, wakiwemo LATRA, TABOA na Shirika la Posta Tanzania, pamoja na wasanii, waigizaji na wanatasnia walioshiriki katika utayarishaji wa filamu hiyo.
Uzinduzi wa filamu “Kifurushi” umeenda sambamba na kaulimbiu isemayo: “Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya.”




