FA

B19 yajipanga kuing’oa Simba Kombe la Shirikisho

DAR ES SALAAM: TIMU ya Championship ya B19 imepania mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba ikisema imeweka fungu maalum ili kuiondosha Simba katika hatua hiyo ya 32 bora.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu ya B19, Felix Makota, amesema amesema wanautambua ugumu wa mchezo huo dhidi ya moja ya timu kubwa nchini, lakini hilo halijawakatisha tamaa, badala yake limewapa motisha zaidi ya kupambana na kuandika historia.

“Tunaifahamu Simba ni timu kubwa na yenye uzoefu, ndio maana uongozi umeamua kuweka dau kwa wachezaji wetu. Hizi mechi sio za kwenda uwanjani kawaida, zinahitaji moyo, ari na kujitoa kwa asilimia mia moja,” amesema Makota.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Makota amesema kuwa mchezo huo ni muhimu kwa wachezaji wao kuonesha vipaji vyao mbele ya taifa, akisisitiza kuwa ni nafasi ya “kujiuza” na kuitangaza timu.

“Ni mechi muhimu sana kwa wachezaji wetu. Waitumie kama sehemu ya kujiuza, lakini pia kuitangaza timu yetu. Mechi za mtoano kama hizi zinaweza kubadili historia ya mchezaji na klabu kwa dakika tisini tu,” amesema.

“Watu wengi wanaamini tunaenda kufungwa, lakini niwaambie wazi kabisa tunaenda kuishangaza Tanzania. Wachezaji wamejipanga, uongozi umeliona hilo na kila mmoja yupo tayari kupambana hadi dakika ya mwisho,” amesisitiza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button