Nyumbani

Azam kufungua nafasi zaidi kwa michezo

DAR ES SALAAM: WINGI wa mashindano ya soka, kriketi na mpira wa kikapu yanayochezwa kwa wakati mmoja ni sababu ya Azam TV kuongeza channel nyingine ya michezo, Azam Sports 5 HD, ili kutoa fursa ya kurusha michezo zaidi kwa mashabiki.

Uzinduzi wa chaneli hiyo umefanyika wakati Azam TV ikianza kampeni ya “Tisa Kumi, Moto Juu ya Moto”, huku kampuni hiyo ikieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na kukua kwa mahitaji ya maudhui ya michezo na wingi wa mashindano yanayochezwa kwa wakati mmoja.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa chaneli hiyo, Meneja wa Matangazo, Matukio na Media wa Azam TV, Sebastian Mwaikambe, amesema ongezeko hilo limelenga kuhakikisha wapenzi wa michezo hawakosi matukio kutokana na kugongana kwa ratiba.

“Tumewasikia wanamichezo na tunataka kuwapa fursa ya kuonesha vipaji vyao. Tuna soka, tuna kriketi, tuna kikapu. Kuna wakati tunaweza kuonesha mechi zaidi ya kumi kwenye channel zetu zote,” amesema Mwaikambe.

Amesema awali baadhi ya maudhui yalikuwa yakikosa nafasi kutokana na wingi wa michezo, hivyo kuanzishwa kwa Azam Sports 5 HD kutaongeza uwezo wa kituo hicho kurusha matukio mengi zaidi kwa wakati mmoja.

Mkuu wa Masoko wa Azam TV, Gloria Chuwa, amesema Azam Sports 5 HD imeongeza wigo wa maudhui ya michezo, huku akieleza kuwa lengo ni kuwafikishia watazamaji michezo mingi zaidi.

“Kwa kuongezeka kwa chaneli hii, maana yake imeongeza wigo mpana wa kuongeza maudhui mengi zaidi ya michezo,” amesema Chuwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko wa Azam Pesa, Hussein Simba, amesema ushirikiano wao na Azam TV katika kampeni hiyo unalenga kuwawezesha wateja kupata huduma huku wakiendelea kufuatilia maudhui mbalimbali ya michezo na burudani.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button