Maonesho ya Kanye West Russia yafutwa

MOSCOW: MAONESHO mawili ya mwanamuziki wa Marekani, Kanye West, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika jijini St Petersburg, Russia, mwezi Oktoba yameghairishwa rasmi.
Kwa mujibu wa mwandaaji wa maonesho hayo, Say Agency, maonesho hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Oktoba 10 na 11 hayatafanyika kama ilivyopangwa.
Taarifa hiyo ilitolewa baada ya wiki kadhaa za sintofahamu kuhusu hatima ya maonesho hayo.
Say Agency haikutoa sababu ya moja kwa moja ya kughairiwa kwa maonesho hayo, huku ikisema itatoa taarifa zaidi kuhusu hatua zinazofuata katika siku zijazo. Waandaaji pia wamesema taarifa kuhusu kurejeshwa kwa fedha za tiketi zitatolewa.
Awali, maonesho hayo yalipangwa kufanyika katika Gazprom Arena, lakini uongozi wa uwanja huo ulisema haukuwa umesaini mkataba wa kukodisha eneo hilo kwa ajili ya maonesho ya Kanye West, hali iliyozidisha sintofahamu kuhusu tukio hilo.
Kanye West alitarajiwa kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa wa kimataifa kufanya maonesho nchini Russia tangu mwaka 2022.
Hata hivyo, mpango huo ulikabiliwa na mijadala na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi na makundi nchini humo kutokana na kauli zake za nyuma.
Kufuatia kughairiwa kwa maonesho hayo, Kanye West bado hajatoa kauli yake binafsi kuhusu uamuzi huo. Waandaaji kwa sasa wameahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu hatima ya mpango huo na taratibu za kurejesha fedha kwa watu walionunua tiketi.




