Arsenal yabanwa 2-2, Bayern na Juventus zapiga 3-0

PARIS: TIMU ya wanawake ya Arsenal, ambao walitwaa ubingwa mwaka 2025, walishindwa kuendelea kuongoza kwa mabao mawili na kulazimishwa sare ya 2-2 na Paris FC.
Alessia Russo na Georgia Stanway waliifungia Arsenal mabao yaliyowapa uongozi, lakini Clara Mateo aliipunguzia Paris FC bao moja dakika ya 71.
Mchezo huo uligeuka dakika za mwisho baada ya nahodha wa Arsenal, Leah Williamson, kuadhibiwa kwa penalti kufuatia tukio ambalo mwamuzi Iuliana Demetrescu aliamua mpira ulikuwa tayari umechezwa kabla Williamson kuushika kwa mkono.
Maeline Mendy akafunga penalti hiyo na kuifanya Paris FC kusawazisha 2-2.
Katika mchezo mwingine, OL Lyonnes walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Chelsea baada ya VAR kuingilia kati katika matukio mawili yaliyoweza kuzaa penalti kwa wenyeji. Chelsea nao walifunga bao kupitia Salma Paralluelo, lakini likakataliwa kwa sababu ya kuotea.
Bayern Munich waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Benfica, huku Klara Buehl, Pernille Harder na Franziska Kett wakifunga mabao hayo. Nayo Juventus ilirejea kwenye ushindi baada ya kuifunga Hacken ya Sweden mabao 3-0.




