Kwingineko

Jezi ya Ronaldo ‘yataifishwa’ Ureno

COPENHAGEN: MPYA kutoka kambi ya timu ya taifa ya Ureno ni kuwa namba saba ya mkongwe Cristiano Ronaldo sasa imekabidhiwa kwa Rafael Leao.

Hilo limebainika baada ya Ureno kuanika orodha ya namba za wachezaji watakazozitumia kuelekea mechi yao ya usiku wa leo dhidi ya Denmark katika mwendelezo wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya.

Mshambuliaji huyo wa Galatasaray amepewa namba hiyo ikiwa ni siku moja imepita tangu kuondoka kwa Ronaldo, 41 ambaye ni nahodha wa kikosi hicho.

Ronaldo aliondoka katika kambi hiyo kwa kilichodaiwa kocha Jorge Jesus kutokuwa na mpango wa kumuanzisha kwenye mechi ya Denmark.

Lakini pia kwenye mechi iliyopita dhidi ya Norway walioibuka na ushindi wa mabao 2-1, Ronaldo alinyanyuliwa kutoka benchi apashe misuli lakini hakuingia katika mchezo huo.

Straika huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus, alianzishwa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Wales waliyoshinda bao 1-0. Katika mechi hiyo alitolewa dakika ya 67 na nafasi yake kuchukuliwa na Goncalo Ramos.

Ronaldo anayekipiga Al-Nassr ya Saudia ameeleza taarifa ya kuondoka kambini ipo katika shirikisho la soka la nchi hiyo na siku moja atafafanua kwa nini alichukua uamuzi huo.

Aidha, baada ya Leao kupewa namba saba, straika wa Borussia Dortmund, Fabio Silva amejumuishwa kuziba pengo la Ronaldo na kurithi namba 17 iliyokuwa ikivaliwa na Leao hapo awali.

Wakati huohuo, kiungo Bruno Fernandez aliyeikosa mechi ya Norway kutokana na majeraha, leo anatarajiwa kuwepo uwanjani akiripotiwa kupona majeraha hayo.

Related Articles

Back to top button