Ligi Daraja La Kwanza
Asikwambie mtu, kuaga kunaumiza bwana!

MEXICO CITY:SAFARI ya kipekee ya Guillermo Ochoa katika soka la kimataifa imekaribia kufikia mwisho baada ya golikipa huyo kuonekana kwa mara ya mwisho katika Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Mexico.

Ochoa mwenye umri wa miaka 40 aliingia uwanjani katika Kombe lake la Dunia la sita, hatua inayomuweka miongoni mwa wachezaji wachache sana waliowahi kufikia mafanikio hayo katika historia ya mashindano.
Golikipa huyo tayari amethibitisha kuwa atastaafu soka baada ya Kombe la Dunia 2026, jambo lililofanya kuonekana kwake katika mchezo huo kuwa tukio maalumu kwa mashabiki wa Mexico na wapenda soka duniani.

Baada ya mchezo, Ochoa alieleza hisia zake kwa kusema kuwa mechi yake ya kwanza kabisa ya soka la kulipwa ilichezwa katika Uwanja wa Azteca na sasa mechi yake ya mwisho imechezwa katika uwanja huohuo.
Kauli hiyo iligusa hisia za mashabiki wengi ambao wamekuwa wakimshuhudia kwa zaidi ya miaka 20 akiwa miongoni mwa nyota wakubwa wa soka la Mexico.
Katika matoleo mbalimbali ya Kombe la Dunia, Ochoa amejijengea sifa ya kuwa mmoja wa makipa waliowahi kuwa na viwango bora zaidi, mara nyingi akiwa shujaa wa Mexico katika mechi kubwa dhidi ya mataifa makubwa duniani.




