EPL

Arsenal yainufaisha Ligi Kuu ya England

LONDON, Ligi Kuu England (EPL) imehakikishiwa kuwa na timu tano zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, baada ya kupata rasmi nafasi ya ziada ya Ulaya maarufu kama European Performance Spot (EPS) kwa mwaka wa pili mfululizo.

Nafasi hiyo ilipatikana jana usiku baada ya Arsenal kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sporting katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Champions League.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), nafasi mbili za ziada hutolewa kwa ligi mbili zitakazofanya vizuri zaidi katika mashindano matatu ya Ulaya ambayo ni Champions League, Europa League na Conference League.

Msimu huu, Epl imekuwa ikiongoza katika jedwali la pointi za ubora wa mashindano ya Ulaya, huku timu zote tisa zilizoiwakilisha England zikifanikiwa kutinga hatua ya 16 bora.

Ingawa ni timu tano pekee zilizofanikiwa kufuzu robo fainali, pointi walizokusanya katika hatua za awali tayari ziliiweka England katika nafasi nzuri ya kupata tiketi hiyo ya ziada.

Kutokana na hilo, sasa ni rasmi kuwa timu itakayomaliza nafasi ya tano katika Premier League msimu huu nayo itafuzu moja kwa moja kushiriki Champions League msimu ujao.

Kwa sasa, Liverpool ndiyo inayoshikilia nafasi hiyo ya tano ikiwa na pointi 49, lakini ushindani wa nafasi hiyo ni mkali mno.

Tofauti ya pointi kati ya Liverpool na Bournemouth walio nafasi ya 13 ni pointi saba pekee, jambo linalomaanisha kuwa mbio za tiketi ya Ulaya bado ziko wazi kwa timu nyingi.

Baada ya Liverpool, nafasi zinazofuata zinashikiliwa na Chelsea wenye pointi 48, Brentford 46, Everton 46, Fulham 44, Brighton 43, Sunderland 43, Newcastle United 42 na Bournemouth 42.

Wakati England ikijihakikishia nafasi hiyo, Hispania inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumaliza ya pili katika msimamo wa alama za ubora wa Ulaya, mbele ya Ujerumani na Ureno.

Hata hivyo, Bundesliga bado ina matumaini ya kufanya mabadiliko ya mwisho baada ya Bayern Munich kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Real Madrid, huku Freiburg pia wakitarajiwa kucheza dhidi ya Celta Vigo katika Europa League.

Iwapo nafasi hizo mbili za ziada zitakwenda kwa Premier League na La Liga, basi itakuwa ni marudio ya msimu uliopita ambapo ligi hizo mbili ndizo zilizoongoza kwa ubora wa uwakilishi wa Ulaya.

Lakini hali inaweza kuwa ya kipekee zaidi kwa England, kwani bado kuna uwezekano wa Premier League kuwa na timu sita au hata saba katika Champions League msimu ujao.

Iwapo Aston Villa, ambao kwa sasa wako nafasi ya nne na pointi 54, watafanikiwa kutwaa Europa League lakini wakamaliza nje ya nne bora, basi England itapata timu ya sita katika Champions League.

Hali kama hiyo inaweza pia kutokea kwa Liverpool, ambao wanatarajiwa kucheza dhidi ya Paris Saint-Germain katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Champions League.

Kama timu yoyote itatwaa taji la Ulaya na kisha ikamaliza nafasi ya tano, basi timu ya sita kwenye msimamo nayo inaweza kufuzu kupitia nafasi hiyo ya ziada.

Na kama kutatokea timu mbili zikashinda mataji ya Ulaya huku zikimaliza nafasi ya tano na sita, basi hata nafasi ya saba inaweza kufuzu kwa Champions League.

Aidha, Nottingham Forest nao bado wako hai katika robo fainali ya Europa League, na wana nafasi ya kuiga yaliyofanywa na Tottenham msimu uliopita kwa kutwaa taji hilo huku wakimaliza katika nusu ya chini ya msimamo wa ligi.

Endapo hilo litafanyika, Premier League inaweza tena kushuhudia idadi kubwa ya timu zake zikitinga mashindano makubwa zaidi ya klabu barani Ulaya.

Kwa sasa, macho ya wengi yataelekezwa katika mbio za nafasi ya tano, sita na hata saba.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button