Aggy Simba: Sina baya na kiongozi yoyote Simba SC

MWANACHAMA wa klabu ya Simba SC, Agnes Daniel maarufu ‘Aggy Simba’ amesema hajawahi kukosana na kiongozi yoyote wa klabu hiyo.
Akipiga stori na SpotiLEO, mapema hii leo, mwanachama huyo amesema kama mwanachama kikatiba ni haki yake kuhoji anapoona baadhi ya mambo ya klabu hayako kwenye mstari.
Hatua hiyo imekuja baada ya Juni 15, 2024 Sekretarieti ya klabu hiyo kuwasimamisha wanachama wawili Mohammed Khamis Mohammed na Agnes Daniel mpaka pale kamati ya maadili itakapoamua vinginevyo.
Mwandishi wa mtandao huu ulimsaka Aggy Simba kutaka kufahamu sababu zilizopelekea kusimamishwa na je nini kitafuata baada ya hapo.
Akijibu swali hilo, Aggy Simba ameiambia SpotiLEO kuwa hafahamu sababu za kusimamishwa hivyo anasubiri kuitwa kwenye kamati kuona itaamuaje.
“Nimeona barua kwenye mitandao ya kusimamishwa kwangu kwasababu zilizotajwa na wao, pia barua imesema tutaitwa kamati ya maadili na mimi nasubiri kuitwa kwenye kamati ya maadili ili nijue makosa yangu ni yapi kikatiba,” amesema Aggy Simba.
SpotiLEO iliataka kufahamu kama anatamani siku moja kuwa kiongozi wa timu hiyo ambapo amesema kwasasa hafikirii hilo kwani anafurahia zaidi kuwa mwanachama.