Nyumbani

Singida yapunguza mzigo wa kikosi

DAR ES SALAAM: SINGIDA Black Stars imeanza kupunguza idadi ya wachezaji wake baada ya kubaini kuwa wingi wa kikosi ulikuwa changamoto katika upangaji wa timu na ugawaji wa nafasi za kucheza, hatua inayolenga kuongeza ushindani na utulivu ndani ya kikosi hicho.

Msemaji wa klabu hiyo, Hussein Massanza, amesema leo kuwa tathmini iliyofanyika ilionesha kuwa idadi ya wachezaji ilikuwa kubwa kuliko mahitaji ya benchi la ufundi, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto kwa kocha katika kupanga kikosi cha kila mchezo.

Amesema awali klabu ilitumia fursa ya kanuni kuruhusu usajili wa wachezaji 25 kutokana na kushiriki mashindano mbalimbali, ikiwamo Ligi Kuu , Kombe la Shirikisho la CRDB na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, Massanza amesema baadaye walibaini kuwa wingi huo ulianza kuleta changamoto ya kuwapa wachezaji nafasi za kucheza na kuathiri utulivu wa kikosi kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya wachezaji wanaotumika.

“Moja ya changamoto kubwa tuliyoibaini ni wingi wa wachezaji. Tulikuwa na wachezaji wengi kuliko mahitaji ya kiufundi, ndiyo maana tathmini ikafanyika na kuanza kuchukua hatua. Wale walioondoka wameondoka vizuri kwa makubaliano ya pande zote mbili,” amesema.

Amesema hatua hizo zimeanza kuleta nafuu kwa sababu wachezaji waliobaki sasa wana imani kubwa ya kupata nafasi ya kucheza na kuonesha uwezo wao, huku benchi la ufundi likipata nafasi ya kufanya kazi kwa utulivu zaidi.

Massanza amefafanua kuwa mabadiliko hayo hayakufanywa na uongozi pekee, bali yalihusisha pia tathmini ya kiufundi pamoja na mapendekezo ya kocha Papy Kimoto na benchi lake la ufundi.

Amesema kocha alifurahishwa na hatua ya uongozi kusikiliza mapendekezo yake, akieleza kuwa na wachezaji wanaokidhi mahitaji ya kiufundi ni muhimu zaidi kuliko kuwa na idadi kubwa ambayo inakuwa vigumu kuitumia kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa kwa sasa kikosi kinaendelea na maandalizi kwa ajili ya kurejea kwenye Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku dhamira ikiwa ni kufanya vizuri katika mashindano yote mawili.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button