Terrence apokea waigizaji wa A.I kwa mikono miwili

CALIFORNIA: GWIJI wa filamu, Terrence Howard amesema zama za dhahabu za Hollywood zinaelekea ukingoni na sasa ni zamu ya waigizaji wa A.I (akili mnemba).
Ingawa wengi wana hofu na hilo, lakini Terrence anaamini hilo si jambo baya kimsingi.
Mkongwe huyo alifafanua hayo alipokuwa akihojiwa baada ya hafla ya filamu yake mpya, A Good Hand Wasted, na alisema kasi ya utengenezaji filamu inapungua na kubainisha kuwa huo ni mustakabali mbaya kwa waigizaji.
Terrence alisema fursa za uigizaji zinatoweka kabisa, akionya kuwa tunashuhudia mwisho wa zama fulani, sawa na ilivyokuwa wakati wa mpito kutoka kwenye filamu zisizo na sauti kwenda kwenye filamu zenye sauti.
“Huwezi kushindana na jambo lisiloepukika na mabadiliko haya si lazima yawe mabaya, hata kama kuna baadhi ya vipaji vikubwa vitaachwa nyuma,” alisema Terrence.
Pia, alitolea mfano makubaliano yanayoripotiwa kumhusisha mwigizaji, Ben Affleck na Netflix, yenye thamani ya Dola milioni 587 yanayohusu teknolojia ya A.I kama ushahidi kwamba tasnia hiyo tayari inajiandaa kwa mabadiliko hayo.
Hata hivyo, hajakata tamaa kabisa na utengenezaji wa filamu, akisema kuwa mustakabali upo katika kuwaunga mkono watengenezaji filamu na wasanii wanaojitegemea, hasa wakati ambapo studio kubwa zinazidi kukumbatia teknolojia ya A.I.




