Maresca: Foden anaweza kuwa nyota bora EPL

ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Enzo Maresca, amesema ana jukumu la kumsaidia kiungo mshambuliaji Phil Foden kurejea katika kiwango chake bora baada ya nyota huyo wa England kuvunja ukame wa mabao uliodumu kwa miezi 10.
Foden, mwenye umri wa miaka 26, alianza kurejea katika makali yake baada ya kufunga bao katika ushindi wa Manchester City wa mabao 3-2 dhidi ya Ipswich mwishoni mwa wiki iliyopita, kabla ya kuibuka na hat-trick katika ushindi wa 5-1 dhidi ya AEK Athens kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Maresca amesema anaamini Foden ana uwezo wa kurejea katika kiwango kilichomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika Ligi Kuu England.
Foden aliibuka na tuzo kadhaa binafsi katika msimu wa 2023/24 baada ya kufunga mabao 27, lakini amekuwa akipambana kurejesha kiwango hicho katika misimu miwili iliyopita.
Kocha huyo wa Italia, ambaye alichukua mikoba ya kuinoa City mwezi Juni, amesema amekuwa akifanya mazungumzo na Foden ili kumweleza umuhimu wake ndani ya kikosi hicho.
“Tangu tulipoanza kazi, nimekaa na Phil mara mbili au tatu, hasa mwanzoni. Nilitaka kumwonesha jinsi alivyo muhimu kwetu,” alisema Maresca.
Ameongeza kuwa anamfahamu Foden kwa muda mrefu na anaelewa kuwa sababu mbalimbali zimechangia kushuka kwa kiwango chake katika miaka ya hivi karibuni.
“Unapokuwa na wachezaji wengi kama Phil wanaopatikana na kucheza vizuri, unakuwa na timu bora zaidi. Ni suala la kuboresha wachezaji. Ukiwaboresh¬a wachezaji, unaiboresha timu,” alisema.
“Kwangu mimi, ninaona ni wajibu wangu kujaribu kumsaidia Phil awe tena miongoni mwa wachezaji bora zaidi England.”
Foden amewahi kuzungumzia changamoto alizopitia kuhusu afya yake ya akili, huku kiwango chake kikishuka katika kipindi ambacho sasa kocha wake anajaribu kumsaidia kurejea katika ubora wake.
Licha ya kukabiliwa na changamoto ya kumrithi Pep Guardiola, aliyekuwa akiinoa Manchester City kwa takribani miaka 10, Maresca ameanza vizuri katika uongozi wake.
Kocha huyo amekuwa wa kwanza katika historia kushinda mechi zake saba za kwanza za Ligi Kuu England akiwa na klabu mpya.
Hata hivyo, mwanzo huo mzuri umefunikwa kwa kiasi na tuhuma za ukiukaji mkubwa wa kanuni za kifedha za Premier League zinazokabili klabu hiyo.
Manchester City inakabiliwa na uwezekano wa kupewa adhabu kali, ikiwemo kukatwa pointi nyingi, jambo ambalo linaweza kuathiri nafasi yake katika ligi na hata kusababisha kushushwa daraja, kutegemea matokeo ya rufaa yake dhidi ya hukumu inayohusiana na zaidi ya tuhuma 100.




