
CHINA: FILAMU ya kwanza nchini China iliyotengenezwa kikamilifu kwa kutumia akili mnemba (AI), ‘Sanxingdui: Future Past,’ imekabiliwa na mapokezi hafifu kabla ya kuanza kuoneshwa rasmi katika kumbi za sinema, licha ya gharama kubwa ya utayarishaji iliyozidi dola milioni 1.5.
Filamu hiyo ya kusisimua ya kisayansi (sci-fi thriller) imegharimu zaidi ya yuan milioni 10, sawa na takribani dola milioni 1.5, na ilichukua zaidi ya miaka miwili kukamilika, huku karibu watu 100 wakihusika katika utayarishaji wake.
Hata hivyo, takwimu za mauzo ya tiketi kabla ya kuanza kuonyeshwa zimeibua maswali kuhusu uwezo wa filamu zinazotengenezwa kwa AI kuvutia watazamaji wanaolipa ili kuzitazama.
Kwa mujibu wa jukwaa la mauzo ya tiketi la Maoyan, mapato ya tiketi zilizouzwa mapema hadi Alhamisi jioni yalikuwa yuan 65,000 pekee, sawa na takribani dola 9,700.
Maoyan pia ilikadiria kuwa mapato yote ya filamu hiyo katika kumbi za sinema yanaweza kubaki chini ya yuan 100,000, kiasi kidogo mno ikilinganishwa na gharama yake ya utayarishaji.
Filamu hiyo ilipangwa kuanza kuoneshwa rasmi Oktoba 23, 2026, huku zaidi ya maonesho 10,000 yakipangwa kwa siku yake ya kwanza, kwa mujibu wa Maoyan.
Licha ya idadi hiyo ya maonesho, mwitikio wa watazamaji umekuwa mdogo kuliko matarajio, hali inayoiweka sekta ya teknolojia ya China katika mtihani wa kuonesha kama ubunifu wa AI unaweza kuleta mafanikio ya kibiashara katika tasnia ya filamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utayarishaji ya Bona Film Group, Jiang Defu, amekiri kuwa mapokezi ya awali hayajawa ya kuridhisha, lakini akasisitiza kuwa filamu hiyo ni hatua muhimu katika matumizi ya teknolojia mpya.
“Sisi ndio wa kwanza kujaribu, wa kwanza kupata kibali cha kuoneshwa katika kumbi za sinema na wa kwanza kupimwa na watazamaji,” alisema Jiang katika mahojiano na chombo cha habari cha tasnia ya filamu nchini China, Yuli.
Matumizi ya akili mnemba katika utengenezaji wa filamu yamezua mjadala mkubwa kimataifa, hasa kuhusu mustakabali wa ajira kwa waigizaji, waandishi, wahariri na wafanyakazi wengine wa tasnia hiyo.
Nchini Marekani, filamu ya kisayansi iliyotengenezwa kwa AI, Gods Don’t Give Gifts, ilipangwa kutolewa Desemba 4, huku mwigizaji pepe wa Hollywood, Tilly Norwood, akitarajiwa kuonekana katika filamu ijayo iitwayo Misaligned.




