Majeraha yamkosesha mechi Luis Diaz

UJERUMANI: WINGA wa Bayern Munich, Luis Diaz, atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiojulikana baada ya kupata jeraha la misuli ya nyuma ya paja, klabu hiyo ya Ujerumani imethibitisha.
Bayern ilitangaza Alhamisi kuwa nyota huyo wa Colombia amepata mpasuko mdogo wa nyuzi za misuli ya nyuma ya paja la kushoto, hali inayotarajiwa kumuweka nje kwa wiki kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Ujerumani, Diaz anatarajiwa kukaa nje kwa kipindi cha kati ya wiki nne na sita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata jeraha hilo wakati Bayern ilipolazimishwa sare ya mabao 2-2 na Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano.
Diaz aliingia akitokea benchi zikiwa zimesalia zaidi ya dakika 20 kabla ya mchezo kumalizika, lakini alilazimika kutolewa muda mfupi kabla ya filimbi ya mwisho.
Bayern ilieleza kuwa vipimo vilibaini jeraha hilo la misuli, huku hali yake ikimaanisha kuwa hatapatikana kwa michezo ijayo kwa kipindi ambacho bado hakijabainishwa rasmi.
Kabla ya mchezo dhidi ya Arsenal, kocha wa Bayern, Vincent Kompany, alikuwa amefichua kuwa Diaz hakuwa amefanya mazoezi kwa kiwango kamili kuelekea pambano hilo.
Jeraha hilo ni pigo kwa Bayern, ambayo imekuwa ikimtegemea winga huyo katika mashambulizi yake tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Liverpool mwaka 2025.




