Tour De France 2027 kuishia mlima Volkano

MASHINDANO ya baiskeli ya wanawake ya Tour de France Femmes ya mwaka 2027 yanatarajiwa kuhitimishwa kwenye mlima wa volkano wa Puy de Dôme nchini Ufaransa, waandaaji wa mashindano hayo, Amaury Sport Organisation (ASO), wametangaza.
Mashindano hayo yataanza Julai 30 hadi Agosti 7, 2027, yakihusisha hatua tisa, huku Leeds nchini England ikiwa mwenyeji wa mwanzo wa mashindano hayo kabla ya washiriki kuelekea Ufaransa kwa hatua zinazofuata.
Hatua ya mwisho inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa, huku waendesha baiskeli wakikabiliana na mlima mkali wa Puy de Dôme katika hatua ndefu zaidi ya mashindano hayo, yenye urefu wa zaidi ya kilomita 170.
Hatua tatu za kwanza zitafanyika nchini England, zikiwemo mbio za kwanza kabisa za kupimana muda kwa timu katika historia ya Tour de France Femmes.
Mashindano hayo ya kupimana muda kwa timu yatapita mbele ya majengo maarufu ya Big Ben na Buckingham Palace jijini London, yakitarajiwa kuongeza msisimko kwa mashabiki wa mchezo huo.
Mkurugenzi wa mashindano hayo, Marion Rousse, amesema waandaaji wamekuwa wakilenga kujumuisha milima yenye historia kubwa katika kila toleo la mashindano hayo.
“Kila mwaka, tunajaribu kutafuta mlima wenye umuhimu wa kipekee katika historia ya Tour,” alisema Rousse akizungumza na AFP.




