Fifa yatenga dola bilioni 6..4 kusaidia mashirikisho 211

ZURICH, Uswisi: SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limetangaza mpango wa kuanzisha mfuko wa maendeleo wenye thamani ya dola bilioni 6.35 kwa kipindi cha miaka minne ijayo, kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya soka duniani.
Mpango huo unalenga kusaidia mashirikisho yote 211 wanachama wa FIFA, huku kila moja likitarajiwa kupata hadi dola milioni 25 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya soka katika nchi zao.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kuboresha miundombinu ya soka, kuendeleza vipaji vya vijana, kuimarisha mashindano ya ndani na kuongeza fursa kwa wachezaji kupata mafunzo bora. Hata hivyo, matumizi halisi ya fedha hizo yatazingatia masharti na vigezo vitakavyowekwa na FIFA.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za FIFA kupunguza tofauti za maendeleo ya soka kati ya mataifa yenye uwezo mkubwa wa kifedha na yale yenye rasilimali chache, hasa katika maeneo ambayo miundombinu na mifumo ya kukuza vipaji bado inahitaji kuimarishwa.
Iwapo mpango huo utakamilika na kutekelezwa kama ulivyopendekezwa, mashirikisho wanachama yatapata nafasi ya kuongeza uwekezaji katika soka la vijana, soka la wanawake, mafunzo ya makocha pamoja na kuboresha viwango vya waamuzi na wataalamu wengine wa mchezo huo.
Pendekezo hilo linatarajiwa kukamilishwa katika kikao cha Baraza la FIFA mwezi Desemba, wakati maandalizi ya uchaguzi wa urais wa FIFA yakiendelea na muda wa mwisho wa kuwasilisha wagombea ukiwa Novemba 18.




