Muziki

Malaika Gray aingia Warner, aanza na Marioo

DAR ES SALAAM: MSANII chipukizi wa muziki nchini, Malaika Gray, ameanza safari ya kitaalamu katika muziki wa kimataifa baada ya kusainiwa na Africori, kampuni ya usambazaji na huduma za wasanii iliyo chini ya Warner Music Group, huku akianza ukurasa huo kwa kushirikiana na Marioo katika wimbo wake wa kwanza, My Fever.

Wimbo huo unatarajiwa kutoka Oktoba 30 mwaka huu, ukiwa sehemu ya hatua mpya ya Malaika katika kutimiza azma yake ya kuitangaza Tanzania kupitia muziki na utamaduni wake katika soko la kimataifa.

My Fever umeandikwa kwa ushirikiano kati ya Malaika na Marioo, huku utayarishaji ukifanywa na Abbah Process. Wimbo huo ulirekodiwa Tanzania na kuunganisha ladha za Afrobeats na Bongo Flava, pamoja na athari za muziki wa R&B na pop zinazotokana na mazingira ya kimataifa aliyokulia msanii huyo.

Ushirikiano na Marioo unaweka jina la msanii huyo chipukizi pamoja na mmoja wa wasanii wanaojulikana katika muziki wa Bongo Flava, huku video rasmi ya wimbo huo ikitarajiwa kuonesha mandhari mbalimbali za Dar es Salaam chini ya mwongozaji Joma, ambaye alifanya kazi hiyo huku Marioo akishiriki katika utengenezaji wake.

Akizungumzia hatua hiyo, Malaika amesema amekuwa na ndoto ya kuingiza ladha za muziki wa Tanzania katika kazi zake, ikiwamo midundo ya Kiafrika na matumizi ya Kiswahili katika uandishi wa nyimbo, ili kuutambulisha utambulisho wa nchi katika majukwaa ya kimataifa.

Amesema kufanya kazi na Marioo kumekuwa na maana ya kipekee kwake kutokana na namna anavyothamini muziki wa msanii huyo na mchango wake katika muziki wa Tanzania na Afrika Mashariki.

Malaika amekulia Tanzania na Afrika Kusini na kwa sasa anasomea taaluma ya uimbaji na biashara ya muziki katika Chuo cha Muziki cha Berklee kilichopo Boston, Marekani.

Mchanganyiko huo wa elimu ya muziki na uzoefu wa kukulia katika mazingira tofauti unaonekana katika mwelekeo wa kazi yake unaounganisha ladha za ndani na za kimataifa.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Africori, Adam Tiran, amesema Malaika ana sauti na mtazamo wa kipekee unaomtofautisha, akieleza kuwa kampuni hiyo imefurahishwa na nafasi ya kujenga safari yake ya muziki.

 

Related Articles

Back to top button