Adele apaa kasi wimbo wake ‘Nikole Kidman’ wafika Top 10

NEW YORK: MSANII wa muziki wa pop, ADÉLA, ameingia katika 10 bora ya chati ya Billboard Hot 100 nchini Marekani kupitia wimbo wake ‘Nicole Kidman’, uliofikia nafasi ya tisa.
Mafanikio hayo yamemfanya kuwa msanii wa kwanza kutoka Slovakia kufikia hatua hiyo katika chati hiyo maarufu.
Wimbo huo ni miongoni mwa nyimbo zilizomo katika albamu yake ya kwanza ya studio, PRIMA, iliyotolewa Septemba 4, 2026. Tangu wakati huo, wimbo huo umeendelea kupata umaarufu kupitia majukwaa ya kusikiliza muziki na mitandao ya kijamii.
‘Nicole Kidman’ ulianza kuingia katika chati ya Billboard Hot 100 ukiwa nafasi ya 22, kabla ya kupanda hadi nafasi ya tisa. Pia uliripotiwa kufikia nafasi ya kwanza katika chati ya kila siku ya Spotify nchini Marekani, ukiwa na zaidi ya usikilizaji milioni moja kwa siku.
Umaarufu wa wimbo huo umevuka mipaka ya Marekani, ukifikia nafasi ya kwanza nchini Ugiriki na Singapore. Aidha, uliingia katika 10 bora nchini Uingereza, Australia, Canada na Ireland, huku ukishika nafasi ya tatu katika chati ya Billboard Global 200.
Mafanikio hayo yameongezewa nguvu na mwigizaji maarufu wa Hollywood, Nicole Kidman, ambaye alionesha kuupenda wimbo huo hadharani. Mwigizaji huyo alishiriki muziki wa ADÉLA katika chapisho lake la kwanza kwenye mtandao wa TikTok na kuonesha kumuunga mkono kabla ya onyesho la msanii huyo mjini Nashville.
ADÉLA, ambaye baadhi ya mashabiki walimtambua kupitia kipindi cha Netflix cha Dream Academy, anaendelea kujijengea jina kupitia kazi zake za kujitegemea. Mtindo wake wa muziki wa pop, muonekano wa kisanii na namna anavyowasilisha nyimbo zake vimemsaidia kuvutia mashabiki wapya.




